

Lugha Nyingine
China yaitaka Ufilipino kuondoa haraka mfumo wa makombora wa Typhon kama ilivyoahidi hadharani
BEIJING - China inapinga vikali Marekani kuweka mfumo wa makombora wa Masafa ya Kati nchini Ufilipino, na inaitaka Ufilipino kusahihisha makosa yake mapema iwezekanavyo na kuondoa haraka mfumo wa makombora wa Typhon kama ilivyoahidi hadharani, msemaji wa wizara ya mambo ya nje ya China Mao Ning amesema Beijing jana Jumatatu.
Habari zilisema kuwa, jeshi la Ufilipino lilisema jana Jumatatu kwamba limepanga kuweka mfumo wa makombora wa Typhon wa Marekani ili kulinda maslahi yake ya baharini. Kwa kujibu suala hilo, msemaji Mao ameuambia mkutano wa wanahabari siku hiyo ya Jumatatau kwamba China inapinga vikali Marekani kuweka mfumo wa makombora wa Masafa ya Kati nchini Ufilipino, na imetoa upingaji wake huo zaidi ya mara moja.
Msemaji huyo amesma, “ni kitendo cha uchokozi na hatari kwa Ufilipino kuingiza silaha hii ya kimkakati na ya kishambulizi, kitendo hiki ni cha kushirikiana na nguvu ya nje katika kuchochea mivutano na uadui katika kanda hii, na kuchochea mapambano ya siasa za kijiografia na kufanya mashindano ya silaha".
Amesema, kitendo hicho cha uchokozi na hatari, ni chaguo lisilowajibika kabisa kwa watu wa nchi yake na watu wa nchi zote za Asia Kusini Mashariki, hata kwa historia, na usalama wa kikanda.
Msemaji huyo amesema, "Kanda hii inahitaji amani na ustawi, siyo mfumo wa makombora au mapambano. Kwa mara nyingine, tunaihimiza Ufilipino kusikiliza kwa makini wito wa nchi za kanda yetu hii na watu wao, kusahihisha makosa yake mapema iwezekanavyo, kuondoa haraka mfumo wa makombora wa Typhon kama ilivyoahidi hadharani, na kuacha kwenda zaidi chini kwenye njia potofu".
people.cn © Tovuti ya Gazeti la Umma