

Lugha Nyingine
Baraza la Usalama laeleza "wasiwasi mkubwa" juu ya kuzorota kwa hali ya migogoro nchini Haiti
Wawakilishi wakipiga kura juu ya mswada wa azimio katika mkutano wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kwenye makao makuu ya Umoja wa Mataifa mjini New York, Septemba 30, 2024. (Manuel Elias/Picha ya Umoja wa Mataifa/kupitia Xinhua)
UMOJA WA MATAIFA - Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa Jumatatu limeelezea "wasiwasi mkubwa" juu ya hali ya kuzorota kwa migogoro nchini Haiti, likilaani kuendelea kwa ghasia za magenge na kutoa wito wa mshikamano na watu wa Haiti.
Katika taarifa yake kwa vyombo vya habari, wajumbe wa Baraza la Usalama wamesisitiza wasiwasi wao mkubwa juu ya hali inayoendelea kuzorota ya kisiasa, kiuchumi, kiusalama na haki za binadamu, ukosefu wa usalama wa chakula na janga la lishe nchini Haiti.
Baraza hilo vilevile limeeleza wasiwasi wake juu ya vizuizi vya ufikiaji wa misaada ya kibinadamu, na kusisitiza dhamira ya jumuiya ya kimataifa kuendelea kuunga mkono watu wa Haiti.
Wajumbe wa baraza hilo wamelaani vikali vitendo vya kihalifu vinavyoendelea kudhoofisha utulivu vinavyofanywa na makundi yenye silaha na kusisitiza kuwa jumuiya ya kimataifa inapaswa kufanya juhudi zaidi kutoa misaada ya kibinadamu kwa watu wa Haiti na kuunga mkono Jeshi la Polisi la Taifa la Haiti, ikiwa ni pamoja na kujenga uwezo wake wa kurejesha utaratibu wa sheria na utulivu kupitia Ujumbe wa Kuunga Mkono Usalama wa Kimataifa.
Hasa, wamelaani vikali ripoti kwamba makundi yenye silaha yamewaua watu wasiopungua 184 kati ya Desemba 6 na 8 karibu na Wharf Jeremie mji mkuu wa Port-au-Prince.
Nchi wanachama wa baraza hilo zimesisitiza haja ya kujenga mazingira yenye usalama ambayo inasaidia mchakato jumuishi wa kisiasa na uchaguzi huru na wa haki nchini Haiti na kuuhimiza ujumbe huo kuharakisha uwepo wake huko, vilevile kuunga mkono ujumbe huo.
Nchi hizo wanachama wa baraza pia zimeonyesha wasiwasi mkubwa juu ya kuingia kiharamu kwa silaha nchini Haiti ambayo inaendelea kuwa sababu kuu ya hali ya ukosefu wa utulivu na vurugu, na zimetoa wito wa hatua hitajika kutekeleza vikwazo vya silaha.
people.cn © Tovuti ya Gazeti la Umma