China tena yaitaka Ufilipino kuondoa mfumo wa makombora wa Marekani

(Tovuti ya Gazeti la Umma) Desemba 27, 2024

BEIJING - China kwa mara nyingine tena inaitaka Ufilipino kuondoa mfumo wa makombora wa Typhon wa Marekani mapema, kwani kuwekwa kwa mfumo huo kunaleta hatari ya mapambano ya siasa za kijiografia na mashindano ya silaha katika kanda hiyo, msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya China Mao Ning amesema jana Alhamisi.

Mao ametoa maoni hayo kwenye mkutano na waandishi wa habari baada ya Waziri wa Ulinzi wa Ufilipino Gilbert Teodoro kujaribu kuhalalisha hatua ya Marekani kuweka mfumo wa makombora wa Uwezo wa Masafa ya Kati nchini humo. Katika taarifa iliyonukuliwa na vyombo vya habari, Teodoro alisema kuwa hatua yeyote ya kuweka na kununua mali zinazohusiana na usalama na ulinzi ya Ufilipino ni haki yake na mamlaka yake na haipingika na nchi za nje.

Akijibu hilo, Msemaji Mao amesema kuwa China imerudia mara kwa mara upinzani wake thabiti juu ya kuwekwa kwa mfumo huo, akiongeza kuwa mfumo wa makombora wa Typhon, wenye uwezo wa silaha za nyuklia na za kawaida, ni silaha ya kimkakati na ya mashambulizi, badala ya kujihami.

Ufilipino imeshirikiana na Marekani kuweka mfumo huo, ikikabidhi usalama na ulinzi wake wa taifa kwa wengine, ikileta hatari ya mapambano ya siasa za kijiografia na mashindano ya silaha katika kanda hiyo, na kusababisha tishio kubwa kwa amani na usalama wa kikanda, msemaji Mao amesema.

"Hatua hii inaendana na maslahi ya nani, na ni nani anayepaswa kuzungumza kuhusu diplomasia ya kujitegemea? Hili si lolote bali ni hali ya kawaida ya 'kupanga madhara, kupata madhara'," amesema Mao.

Msemaji huyo amesema kuwa Ufilipino imeweka ahadi wazi kwamba haitachukua upande wowote kati ya nchi kubwa, wala kushiriki katika hatua zozote dhidi ya China, na haina nia ya kuzusha mivutano ya kikanda. Wakati huo huo, Ufilipino mara kwa mara imekuwa ikijihusisha na kutumwa kwa vikosi vya kijeshi na kuchochea mapambano katika kanda hiyo kwa kutumia nguvu za nje, Mao ameongeza.

Ufilipino imeeleza hadharani kuwa mfumo huo ulitumika kwa zoezi moja tu la kijeshi la kawaida na kuahidi kuuondoa baada ya zoezi hilo kumalizika Septemba mwaka huu, lakini kisha ukabadili msimamo na kusema kuwa nchi hiyo inataka kuweka mfumo wa kudumu wa makombora na hata inataka kununua. "Huu ni ukosefu wazi wa uaminifu," amesema Mao.

"Kwa mara nyingine tena tunaitaka Ufilipino kuheshimu ahadi zake za awali na kuondoa mfumo huo wa makombora mapema, kama inavyotakiwa na nchi za kikanda, na kuacha kuendelea katika njia potofu," amesema.

(Wahariri wa tovuti:Zhou Linjia,Zhao Jian)

Picha