Vituo 11 vya uvumbuzi wa kiteknolojia vyazinduliwa kwa ajili ya kusukuma ukuaji wa utamaduni na utalii wa China

(Tovuti ya Gazeti la Umma) Desemba 31, 2024
Vituo 11 vya uvumbuzi wa kiteknolojia vyazinduliwa kwa ajili ya kusukuma ukuaji wa utamaduni na utalii wa China
Watu wakifanya onyesho la nyimbo na ngoma za kijadi kwenye tamasha la utalii wa kitamaduni mjini Wuzhou, Mkoa Unaojiendesha wa Kabila la Wazhuang wa Guangxi, kusini mwa China, Novemba 12, 2024. (Xinhua/Huang Xiaobang)

BEIJING - Vituo vipya kumi na moja vya uvumbuzi wa kiteknolojia vimeanza kazi rasmi huku kukiwa na juhudi za kuendeleza sekta ya utamaduni na utalii nchini China, Wizara ya Utamaduni na Utalii ya China imetangaza jana Jumatatu.

Mpango wa kuanzisha vituo hivyo ulizinduliwa mwaka 2023, amesema Liu Dongyan, naibu mkurugenzi wa idara ya sayansi na elimu ya wizara hiyo, katika mkutano na waandishi wa habari.

Kundi la kwanza la vituo hivyo linaanzishwa katika maeneo manane ya ngazi ya mkoa, yakiwemo Beijing, Liaoning, Zhejiang na Fujian. Kwa pamoja, yanaajiri wasimamizi na wataalamu wa kiufundi karibu 1,000, yakiwa na uwekezaji wa jumla zaidi ya Yuan milioni 100 (dola za Kimarekani kama milioni 13.91).

Vituo hivyo vya uvumbuzi vinalenga kutoa huduma mbalimbali za kina kwa kampuni za kitamaduni na utalii, kuziongoza katika kila hatua kuanzia utafiti na maendeleo (R&D) hadi majaribio ya kielelezo na, hatimaye, kugeuza kuwa bidhaa.

Kwa maana ya R&D, vituo hivyo vinajikita katika maeneo matano muhimu ndani ya tasnia za kitamaduni na utalii: vifaa vya maonyesho, vifaa vya michezo, utalii wa kisasa na uendelezaji wa maeneo ya vivutio vya watalii, kuonyesha na kupata uzoefu wa sanaa, na maendeleo ya kidijitali na akili mnemba ya huduma za utamaduni.

Mafanikio muhimu makubwa yaliyopatikana ni pamoja na ushirikiano wa kituo kimoja na maeneo zaidi ya 6,300 ya vivutio vya watalii, ambayo imeuza tiketi zaidi milioni 300 kwa mwaka. Mashirika washirika wa kituo kingine yanashughulikia kuzalisha asilimia zaidi ya 80 ya vifaa vya kuvaa kichwani vya uhalisia pepe (VR) vya kiwango cha kati hadi cha juu duniani.

"Vituo vya uvumbuzi wa kiteknolojia vya wizara hiyo vinatoa mchango mkubwa zaidi katika kuendeleza na kuongoza maendeleo ya teknolojia ya sekta hiyo," Liu amesema.

(Wahariri wa tovuti:Zhou Linjia,Zhao Jian)

Picha