Marais wa Senegal na Cote d'Ivoire watangaza mwisho wa uwepo wa wanajeshi wa kigeni kuanzia mwaka 2025

(CRI Online) Januari 02, 2025

Rais wa Senegal Bassirou Diomaye Faye ametangaza Jumanne "mwisho wa uwepo wa majeshi ya kigeni" nchini humo katika mwaka 2025.

Akizungumza katika hotuba ya Mwaka Mpya, mkuu huyo wa nchi amesema amemuagiza waziri wa jeshi kupendekeza kanuni mpya ya ushirikiano katika ulinzi na usalama, ikihusisha mwisho wa uwepo wa majeshi ya nchi za kigeni nchini Senegal kuanzia 2025 miongoni mwa mambo mengine.

Amewahakikishia wananchi kuwa marafiki wote wa Senegal watachukuliwa kama washirika wa kimkakati ndani ya mfumo wa ushirikiano wa wazi, wa aina mbalimbali na usiozuiliwa.

Wakati huohuo Rais wa Cote d'Ivoire Alassane Ouattara naye pia ametangaza katika salamu zake wa Mwaka Mpya siku ya Jumanne kwamba vikosi vya jeshi la Ufaransa vitaondoka Cote d'Ivoire mapema Januari 2025, akisisitiza kwamba uondoaji huo utakuwa wa "makubaliano na mpangilio."

Amebainisha kuwa Kikosi cha 43 cha Askari wa Majini cha Abidjan (BIMA), kilichopo Port-Bouet, kitongoji cha Abidjan, kitarejeshwa kwa wanajeshi wa Cote d'Ivoire mwezi Januari 2025.

Wanajeshi wa Ufaransa waliokuwepo nchini Cote d'Ivoire wanakadiriwa kufikia 900.

(Wahariri wa tovuti:Song Ge,Zhao Jian)

Picha