

Lugha Nyingine
Ethiopia kuhimiza matumizi ya magari yanayotumia umeme katika miji mingi zaidi
Serikali ya Ethiopia imesema itajaribu kufanya magari mengi zaidi yanayotumia umeme (EVs) kupatikana katika miji yote nchini humo, huku vituo vya kuchajia vikiwa vimewekwa katika maeneo ya Dire Dawa, Harar, na Jigjiga mashariki mwa Ethiopia.
Shirika la Utangazaji la Serikali ya Ethiopia, Fana limewanukuu maafisa wa serikali wakisema Jumatano kwamba juhudi mbalimbali zitaanza ili kufanya magari yanayotumia umeme kuwa mbadala wa magari milioni 1.5 yanayotumia mafuta.
Waziri wa usafirishaji na uchukuzi, Bareo Hassen, amesema mji wa Addis Ababa na mji wa kitalii wa kaskazini wa Gondor tayari imeanza kutumia magari yanayotumia umeme kwa usafiri wa umma.
Hassen ameongeza kuwa Ethiopia inalenga kufanya magari yanayotumia umeme kuwa mbadala wa magari 432,000 yanayotumia nishati ya mafuta katika kipindi cha miaka 10, akibainisha kuwa nchi hiyo imeweza kutumia magari zaidi 100,000 yanayotumia umeme nchini kote katika kipindi cha miaka miwili na nusu iliyopita.
Kama sehemu ya kushinikiza mabadiliko ya kijani, serikali imetangaza kupiga marufuku uagizaji wa magari yanayotumia petroli au dizeli.
people.cn © Tovuti ya Gazeti la Umma