Timu ya madaktari wa China yatoa upasuaji wa mtoto wa jicho bila malipo nchini Ethiopia

(Tovuti ya Gazeti la Umma) Januari 06, 2025
Timu ya madaktari wa China yatoa upasuaji wa mtoto wa jicho bila malipo nchini Ethiopia
Madaktari wa China na daktari wa Ethiopia wakifanya upasuaji wa mtoto wa jicho katika Hospitali ya Tirunesh Beijing mjini Addis Ababa, Ethiopia, Januari 2, 2025. (Hospitali ya Macho ya Tianjin/kupitia Xinhua)

ADDIS ABABA - Timu ya madaktari wa China kutoka Hospitali ya Macho ya Tianjin Ijumaa ilizindua rasmi kampeni ya bila malipo ya upasuaji wa mtoto wa jicho katika Hospitali ya Tirunesh Beijing mjini Addis Ababa, mji mkuu wa Ethiopia.

Chini ya jina la Safari ya Mwangaza ya China na Ethiopia, timu hiyo yenye madaktari waandamizi 10 wa magonjwa ya macho na wauguzi inatarajiwa kufanya upasuaji wa mtoto wa jicho kwa wagonjwa zaidi ya 500, huku 80 kati yao wakiwa tayari wamefanikiwa kufanyiwa upasuaji hadi kufikia Ijumaa.

Balozi wa China nchini Ethiopia Chen Hai amesema katika hafla ya uzinduzi wa kampeni hiyo kuwa kama sehemu ya mpango wa serikali ya China, Hospitali ya Macho ya Tianjin imetuma timu ya wataalamu bora yenye vifaa tiba na teknolojia ya hali ya juu ili kuleta mwanga na matumaini kwa wagonjwa wa Ethiopia.

"Mradi wa 'Safari ya Mwangaza' unaonyesha kidhahiri ushirikiano wetu wa kimkakati wa hali zote na urafiki wa jadi. Mradi huu utasaidia mamia ya wagonjwa wa mtoto wa jicho wa Ethiopia kupata tena uwezo wa kuona," Chen amesema.

Timu hiyo imetoa msaada wa vifaa tiba kwa hospitali hiyo ambayo pia inajulikana kwa jina la Hospitali ya Urafiki wa Ethiopia na China, ambapo madaktari wa China na Ethiopia huhudumia wagonjwa bega kwa bega na kunufaisha ujuzi na uzoefu wa kiufundi wao.

Waziri wa Afya wa Ethiopia Mekdes Daba amesema, Safari ya Mwangaza kati ya China na Ethiopia ina umuhimu mkubwa katika kuendeleza matumaini ya pamoja ya China na Ethiopia kwa kushughulikia si tu ulemavu wa macho bali pia mahitaji ya jamii kwa ujumla.

"Kwa kutoa (huduma ya) upasuaji wa mtoto wa jicho, tutakuwa tukifanya mabadiliko halisi katika kuboresha upasuaji wa macho nchini Ethiopia," Daba amesema, akibainisha kuwa serikali ya Ethiopia inathamini kampeni hiyo ambayo inaendana na sera za afya nchini Ethiopia na kudhihirisha upanuzi wa ushirikiano na matumaini ya pamoja kati ya nchi hizo mbili.

Wa mujibu wa takwimu zilizopatikana kutoka Wizara ya Afya ya Ethiopia, Waethiopia zaidi ya milioni 5.4 wameathiriwa na matatizo mbalimbali ya macho, ambapo nusu yao wanakabiliwa na upofu wa mtoto wa jicho.

(Wahariri wa tovuti:Zhou Linjia,Zhao Jian)

Picha