Lugha Nyingine
China yatoa wito wa kulinda mfumo wa biashara wa pande nyingi unaosimamiwa na WTO
BEIJING - Msemaji wa wizara ya mambo ya nje ya China Guo Jiakun amesema China itaendelea kushirikiana na pande nyingine husika duniani katika kulinda mfumo wa biashara ya pande nyingi, mfumo ambao kiini chake ni Shirika la Biashara Duniani (WTO).
“China itaendelea kuheshimu ahadi zake zilizotoa wakati wa kujiunga na WTO, kuhimiza urahisi wa uwekezaji na biashara huria duniani, na kutoa manufaa zaidi kwa dunia,” Guo ameuambia mkutano na waandishi wa habari jana Jumatatu wakati akijibu swali kuhusu maadhimisho ya miaka 30 tangu kuanzishwa kwa WTO.
Amesema, kupitia kutoa mazingira ya kimfumo yaliyo ya uwazi, utulivu na yanayoweza kukadiriwa, WTO imehakikisha hali ya jumla ya biashara ya kimataifa inaendelea kwa utulivu na kwa utaratibu, na kuimarisha ushirikiano wa kibiashara na kiuchumi kati ya nchi wanachama.
“WTO imeunga mkono nchi zenye uchumi unaoendelea kushiriki na kufaidika na utandawazi wa uchumi, na kutoa mchango muhimu katika kuongeza ustawi wa watu wa nchi mbalimbali na kuhimiza maendeleo endelevu,” ameongeza.
Msemaji huyo akisisitiza kuwa biashara huria ni matakwa ya lazima kwa ukuaji wa uchumi wa dunia, na lengo lake la kimsingi ni kufanya ushirikiano wa kunufaishana na kupata maendeleo kwa pamoja.
"Kujihusisha na kujilinda kibiashara na kujenga 'yadi ndogo, uzio mrefu' kunavuruga vibaya minyororo ya viwanda na minyororo ya utoaji bidhaa ya dunia nzima, na kudhuru maslahi ya pamoja na ya muda mrefu ya nchi zote," amesema.
people.cn © Tovuti ya Gazeti la Umma