

Lugha Nyingine
Waziri Mkuu wa Canada kujiuzulu huku upinzani ukilalamika "hakuna kilichobadilika"
Waziri Mkuu wa Canada Justin Trudeau akizungumza katika Mkutano wa tatu wa Kilele wa Biashara wa Nchi za Amerika mjini Lima, Peru, Aprili 13, 2018. (Xinhua/Xu Rui)
OTTAWA - Waziri Mkuu wa Canada Justin Trudeau ametangaza jana Jumatatu asubuhi kwamba anajiuzulu baada ya uchaguzi wa ndani ya chama chake huku kiongozi wa upinzani akilalamika kwamba hakuna kilichobadilika.
Akitoa hotuba nje ya makazi yake yaliyoko Rideau Cottage, Trudeau amesema ataendelea kuwa Waziri Mkuu hadi mchukuaji nafasi yake atakapochaguliwa.
"Ninakusudia kujiuzulu kama kiongozi wa chama na kama waziri mkuu baada ya chama kumchagua kiongozi wake ajaye kupitia mchakato thabiti wa ushindani wa nchi nzima. Jana usiku, nilimwomba rais wa Chama cha Liberal kuanza mchakato huo," Trudeau amesema.
"Nchi hii inastahili chaguo halisi katika uchaguzi ujao, na imekuwa dhahiri kwangu kwamba kama nitalazimika kupigana vita vya ndani, siwezi kuwa chaguo bora katika uchaguzi huo," Trudeau amesema.
Waziri Mkuu huyo amesema Gavana Mkuu Mary Simon alikuwa amekubali ombi lake la kuahirisha Bunge bila kulivunja hadi Machi 24.
"Hakuna kilichobadilika," Kiongozi wa chama cha Conservative Pierre Poilievre amesema kwenye akaunti yake ya mtandao wa kijamii, akihoji ni nini kimebadilika kwa tangazo hilo la Trudeau.
"Kila Mbunge na mgombea wa Uongozi wa Chama cha Liberal aliunga mkono kila kitu ambacho Trudeau amefanya kwa miaka 9, na sasa wanataka kuwahadaa wapiga kura kwa kubadilisha sura nyingine ya chama cha Liberal ili kuendelea kuwapora Wacanada kwa miaka 4," amesema Poilievre, kiongozi wa kambi rasmi ya upinzani.
Trudeau anakabiliwa na uasi ndani ya kambi yake ya chama tawala na kura za chini za maoni ya umma, ambazo zinaonyesha kuwa chama chake kinaweza kuondolewa madarakani na chama Conservative cha Pierre Poilievre katika uchaguzi, vyombo vya habari vya Canada vimebainisha.
people.cn © Tovuti ya Gazeti la Umma