

Lugha Nyingine
Indonesia na China zatangaza alama ya maadhimisho ya miaka 75 ya uhusiano wa kidiplomaisi wa pande mbili
Wanadiplomasia wa Indonesia na China wakitangaza alama ya kuadhimisha miaka 75 tangu kuanzishwa kwa uhusiano wa kidiplomasia kati ya nchi hizi mbili huko Jakarta, Indonesia, Januari 7, 2025. (Xinhua/Agung Kuncahya B.)
Wanadiplomasia wa Indonesia na China siku ya Jumanne wametangaza alama ya kuadhimisha miaka 75 tangu kuanzishwa kwa uhusiano wa kidiplomasia kati ya mataifa hayo mawili.
Alama hiyo ilisanifiwa na kijana wa Indonesia ambaye alishinda kwenye mashindano ya usanifu yaliyoandaliwa na Ubalozi wa China mjini Jakarta, Ubalozi wa Indonesia mjini Beijing, na Jumuiya ya Sera za Mambo ya Nje ya Indonesia (FPCI).
"Katika mashindano hayo ya usanifu, tunafurahi kuona wabunifu na wapenda sanaa kutoka nchi zote mbili wakishiriki kwa hamasa, huku kukiwa na mawasilisho ya kazi za usanifu zaidi ya 600 kutoka Indonesia pekee. Kwenye kazi za usanifu, kila mshiriki alitumia ustadi wake wa kuonesha kiunganishi cha uhusiano wa kihistoria, mafanikio ya ushirikiano, na matarajio ya pamoja kwa mustakabali mzuri kati ya China na Indonesia," amesema Balozi wa China nchini Indonesia Wang Lutong katika hafla ya kutangaza alama hiyo iliyofanyika katika Nafasi ya China ndani ya Msikiti wa Istiqlal mjini Jakarta.
Balozi wa Indonesia nchini China Djauhari Oratmangun amepongeza mashindano hayo ya usanifu kwa kuonyesha uhusiano wa wenzi wenye nguvu na wa kudumu kati ya nchi hizi mbili.
"Ushirikiano wa pande mbili unaendelea kuleta manufaa kwa watu wa Indonesia," amedhihirisha na akisisitiza umuhimu wa kuimarisha uhusiano katika usalama, uchumi, na mawasiliano ya kitamaduni kati ya watu.
Dino Patti Djalal, mwanzilishi na mkurugenzi mkuu wa FPCI ambaye pia ni mwanadiplomasia wa zamani wa Indonesia, ameelezea matumaini kuhusu maendeleo ya baadaye ya uhusiano wa Indonesia na China.
“Maadhimisho ya miaka 75 tangu kuanzishwa kwa uhusiano wa kidiplomasia si tu hatua muhimu ya urafiki, lakini pia yataweka msingi imara wa maendeleo ya baadaye ya ushirikiano wa pande mbili,” ameongeza.
Indonesia na China zilianzisha uhusiano wa kidiplomasia tarehe 13 Aprili mwaka 1950.
Picha hii ikionesha Alama ya kuadhimisha miaka 75 tangu kuanzishwa kwa uhusiano wa kidiplomasia kati ya Indonesia na China Januari 7, 2025. (Xinhua/Agung Kuncahya B.)
people.cn © Tovuti ya Gazeti la Umma