Mahama aapishwa kuwa rais wa Ghana

(Tovuti ya Gazeti la Umma) Januari 08, 2025

Rais wa Ghana John Dramani Mahama (katikati)

Rais wa Ghana John Dramani Mahama (katikati) akiwa kwenye hafla ya uapisho katika uwanja wa Black Star mjini Accra, Ghana Januari 7, 2025.  (Xinhua/Seth)

ACCRA - Rais wa Ghana John Dramani Mahama amekula kiapo siku ya Jumanne kuwa rais wa nchi hiyo baada ya kushinda uchaguzi wa urais mwezi Disemba mwaka jana.

Umati mkubwa wa raia wa Ghana kutoka makundi mbalimbali, pamoja na wafuasi wa chama chake, walikusanyika katika uwanja wa Black Star mjini Accra, mji mkuu wa nchi hiyo, kushuhudia hafla hiyo kubwa. Hafla hiyo pia ilihudhuriwa na wakuu wa nchi za Afrika na viongozi wengine wa kigeni.

Akihutubia hafla hiyo, Rais Mahama amesema kuwa uapisho huo unaashiria ukurasa mpya katika historia ya Ghana na unatoa fursa adimu ya kuijenga upya nchi hiyo kwa njia mbalimbali.

"Tumepitia matatizo makubwa ya kiuchumi huku tukipita kutoka kwenye msukosuko mmoja hadi mwingine katika miaka ya hivi karibuni. Lakini kuna matumaini juu ya upeo wa macho, na leo ni mwanzo wa fursa mpya, fursa ya kupanga upya mikakati yetu ya utawala na uchumi. Kwa pamoja tunaweza kujenga upya taifa letu pendwa," Mahama amesema.

Ameahidi kuwa serikali yake itashughulikia tatizo la ukosefu wa ajira kwa vijana kwa kujenga na kuendeleza ushirikiano thabiti na sekta binafsi ili kutoa fursa za ajira zenye staha na zinazolipa vizuri.

"Katika ushindi huu mkubwa, naona wito mkubwa, hasa kutoka kwa vijana wa Ghana, na wakati huu ni uthibitisho wenye nguvu kwamba sauti zenu ni muhimu na kwamba mustakabali wenu lazima uwe kipaumbele chetu," amesema.

Akiwa alizaliwa mwaka 1958 katika mkoa wa Savannah wa Ghana, Mahama aliwahi kuwa rais wa Ghana kuanzia mwaka 2012 hadi 2017.

Rais wa Ghana John Dramani Mahama (katikati) akiwa kwenye hafla ya uapisho katika uwanja wa Black Star mjini Accra, Ghana Januari 7, 2025.  (Xinhua/Seth)

John Dramani Mahama (katikati) akila kiapo kuwa rais katika uwanja wa Black Star mjini Accra, Ghana Januari 7, 2025.  (Xinhua/Seth)

(Wahariri wa tovuti:Song Ge,Zhao Jian)

Picha