

Lugha Nyingine
Namibia na China zaahidi kuendeleza matokeo ya Mkutano wa Kilele wa FOCAC wa Beijing
Rais wa Namibia Nangolo Mbumba akikutana na Wang Yi, Waziri wa Mambo ya Nje wa China ambaye pia ni mjumbe wa Ofisi ya Siasa ya Kamati Kuu ya Chama cha Kikomunisti cha China (CPC) mjini Swakopmund, Namibia, Januari 6, 2025. (Xinhua/Zhang Yudong)
WINDHOEK - Rais wa Namibia Nangolo Mbumba Jumatatu alikutana na Wang Yi, Waziri wa Mambo ya Nje wa China ambaye pia ni mjumbe wa Ofisi ya Siasa ya Kamati Kuu ya Chama cha Kikomunisti cha China (CPC) katika mji wa Swakopmund, huku pande zote mbili zikiahidi kuendeleza ushirikiano wa pande mbili.
Licha ya umbali wa kijiografia, uhusiano kati ya China na Afrika umeendelea kuwa imara, amesema Wang.
Uhusiano kati ya China na Afrika umestahimili jaribu la mabadiliko ya mazingira ya kimataifa na unaonyesha matarajio mapya yenye matumaini, amesema, akisisitiza kuwa China inaendelea kuwa mshirika wa kutegemewa wa Afrika, mara zote bila kuyumbayumba ikiipa Afrika kipaumbele katika mkakati wake wa kidiplomasia.
Kwa miaka 35, mawaziri wa mambo ya nje wa China wameifanya Afrika kuwa kituo cha ziara zao ya kwanza nje ya nchi kila mwanzoni mwa mwaka, desturi inayoonyesha dhamira isiyoyumbayumba ya China, Wang amesema, akiongeza kuwa desturi hiyo itaendelea kwa sababu kuimarisha ushirikiano kati ya China na Afrika ni muhimu zaidi kuliko hapo awali kwa dunia, na maendeleo yao ya pamoja yanaashiria kuibuka kwa Nchi za Kusini na kuongezeka kwa ushawishi wa haki.
Katika Mkutano wa Kilele wa Jukwaa la Ushirikiano kati ya China na Afrika (FOCAC) uliofanyika Beijing mwaka jana, Rais Xi Jinping wa China alipendekeza mipango 10 ya ushirikiano ili kuendeleza kwa pamoja ujenzi wa mambo ya kisasa na kutangaza kuwa sifa ya jumla ya uhusiano kati ya China na Afrika imepandishwa ngazi hadi kufikia jumuiya ya China na Afrika ya siku zote yenye mustakabali wa pamoja katika zama mpya.
Rais wa Namibia Nangolo Mbumba akiwasili kwa hafla ya ufunguzi wa Mkutano wa Kilele wa 2024 wa Jukwaa la Ushirikiano kati ya China na Afrika (FOCAC) kwenye Jumba la Mikutano ya Umma mjini Beijing, mji mkuu wa China, Septemba 5, 2024. (Xinhua/Li He)
Haya yamedhihirisha mwelekezo wa maendeleo ya baadaye ya uhusiano kati ya China na Afrika, Wang amesema, akibainisha kuwa China iko tayari kufanya kazi na Namibia kutekeleza mipango kazi hiyo 10 ya ushirikiano, ikisaidia Namibia kuharakisha mchakato wake wa ujenzi wa mambo ya kisasa.
Kwa upande wake Mbumba amesema licha ya tofauti za ukubwa, Namibia na China siku zote zimedumisha uhusiano wa urafiki, mshikamano na ushirikiano unaozingatia kuheshimiana na kuungana mkono.
Namibia inafuata kithabiti kanuni ya kuwepo kwa China moja, inaunga mkono juhudi za China za kulinda ukamilifu wa ardhi yake, ikiwa ni pamoja na Taiwan, na inahamasika na mafanikio yaliyopatikana chini ya mwongozo wa Fikra ya Xi Jinping juu ya Ujamaa wenye Umaalum wa China katika Zama Mpya na uongozi wa Chama cha Kikomunisti cha China, amesema, akiongeza kuwa Namibia inatarajia kuimarisha mabadilishano ya kati vyama na China na kuchangia uzoefu wa utawala.
people.cn © Tovuti ya Gazeti la Umma