China na Jamhuri ya Kongo kutekeleza matokeo ya FOCAC kwa ajili ya ushirikiano wa karibu zaidi

(Tovuti ya Gazeti la Umma) Januari 09, 2025
China na Jamhuri ya Kongo kutekeleza matokeo ya FOCAC kwa ajili ya ushirikiano wa karibu zaidi
Waziri wa Mambo ya Nje wa China Wang Yi, ambaye pia ni mjumbe wa Ofisi ya Siasa ya Kamati Kuu ya Chama cha Kikomunisti cha China (CPC), akifanya mazungumzo na Waziri wa Mambo ya Nje wa Jamhuri ya Kongo Jean-Claude Gakosso mjini Brazzaville, Jamhuri ya Kongo, Januari 7, 2025. (Xinhua/Zheng Yangzi)

BRAZZAVILLE - Waziri wa Mambo ya Nje wa China Wang Yi amefanya mazungumzo na mwenzake wa Jamhuri ya Kongo Jean-Claude Gakosso siku ya Jumanne, wakiahidi kutekeleza matokeo ya Mkutano wa Kilele wa Beijing wa Baraza la Ushirikiano kati ya China na Afrika (FOCAC) uliofanyika mwaka jana katika juhudi za kuimarisha ushirikiano kati ya China na Afrika.

Kwenye mazungumzo hayo, Wang ambaye pia ni mjumbe wa Ofisi ya Siasa ya Kamati Kuu ya Chama cha Kikomunisti cha China (CPC), amesema kwa muda mrefu imekuwa ni desturi kwa waziri wa mambo ya nje wa China kuifanya Afrika kuwa kituo cha ziara ya kwanza nje ya nchi kila mwanzoni mwa mwaka.

"Desturi hii ya muda mrefu, ambayo inasisitiza mshikamano na ushirikiano wa kudumu kati ya China na Afrika, ni msingi wa sera ya nje ya China na chaguo thabiti la kimkakati." amesema.

Ameongeza kuwa bila kujali hali ilivyobadilika katika mazingira ya kimataifa, China itaendelea kuwa na dhamira ya kuimarisha uhusiano na ushirikiano wake na Afrika.

Akiielezea Jamhuri ya Kongo kama rafiki thabiti wa China, Wang amesema kuwa nchi hizo mbili zimeshirikiana kwa zaidi ya miaka 60 tangu kuanzishwa kwa uhusiano wa kidiplomasia, kwa kuelewana na kuungana mkono kithabiti, na kukabiliana na changamoto kwa pamoja.

Kama mwenyekiti mwenza wa FOCAC, Jamhuri ya Kongo inaonyesha ushirikiano wa ngazi ya juu kati ya nchi hizo mbili na kutoa sauti za Bara la Afrika, Wang amesema, akielezea imani yake kwa Jamhuri ya Kongo kutekeleza kikamilifu majukumu yake kama mwenyekiti, ikitoa mchango katika utekelezaji wa matokeo ya Mkutano wa Kilele wa FOCAC wa Beijing na kuendeleza ushirikiano kati ya China na Afrika.

“Juhudi hizi, si tu zitaimarisha maendeleo ya Jamhuri ya Kongo lakini pia zitaongeza ushawishi wake wa kimataifa” ameongeza Wang.

Kwa upande wake, Gakosso ametoa shukrani zake kwa ziara hiyo ya Wang, hususan nchini Jamhuri ya Kongo, akiielezea kuwa ni ushahidi wa dhamira ya China katika uhusiano wao wa pande mbili.

Licha ya umbali wa kijiografia na tofauti za kitamaduni, Gakosso amesisitiza kuwa nchi hizo mbili zimeunda uhusiano wa kipekee na wa kudumu, yakifanya uhusiano wao kuwa mfano wa kuigwa wa uhusiano wa kimataifa.

(Wahariri wa tovuti:Zhou Linjia,Zhao Jian)

Picha