

Lugha Nyingine
Nchi za Ulaya zajibu kauli ya Trump kuhusu Greenland, yakisisitiza kuheshimu mamlaka
Watu wakicheza kwenye theluji mbele ya Jumba la Taifa karibu na jengo la Bunge la Marekani, Capitol Hill mjini Washington D.C., Marekani, Januari 31, 2021. (Xinhua/Liu Jie)
OSLO - Nchi mbalimbali za Ulaya zimepinga kauli iliyotolewa na Rais mteule wa Marekani Donald Trump kuhusu uwezekano wa kutumia nguvu za kijeshi kutwaa udhibiti wa Greenland, ikiongeza hali ya wasiwasi kuhusu kauli yake ya awali kuhusu eneo hilo linalojitawala la Denmark.
Kwenye mkutano na waandishi wa habari siku ya Jumanne, Trump alisema hataondoa uwezekano wa kuchukua hatua za kijeshi katika eneo la Greenland na Mfereji wa Panama. Hii imesababisha majibu ya haraka kutoka kwa viongozi wa Ulaya, wakisisitiza utakatifu wa mamlaka ya kujitawala na sheria za kimataifa.
Kansela wa Ujerumani Olaf Scholz amesema kuwa kutokiukwa kwa mipaka ni kanuni ya msingi ya sheria ya kimataifa, ambayo inatumika kwa kila nchi, bila kujali ukubwa wake au uwezo wake. Amesema katika majadiliano na washirika wa Ulaya, hakuna maelewano juu ya taarifa hizo za hivi karibuni kutoka Marekani.
Picha hii iliyopigwa tarehe 4 Oktoba 2024 ikionyesha jengo la Kamisheni ya Ulaya mjini Brussels, Ubelgiji. (Xinhua/Zhao Dingzhe)
Waziri Mkuu wa Denmark Mette Frederiksen amesisitiza kwamba mustakabali wa Greenland uko mikononi mwa wakaazi wake pekee. "Greenland imeweka wazi kuwa si ya kuuzwa," amesema.
Waziri Mkuu wa Greenland Mute Egede ameunga mkono maoni haya. "Greenland ni ya Wagreenland. Mustakabali wetu ni juu yetu kuutengeneza," ameandika katika ujumbe wake kwenye mtandao wa Facebook.
Siku ya Jumanne, Donald Trump Jr., mtoto mkubwa wa Trump, alitembelea Nuuk, mji mkuu wa Greenland, akielezea safari hiyo kuwa ziara ya kibinafsi ya utalii. "Tuko hapa kama watalii tu, kuona yote," aliwaambia waandishi wa habari, akikataa kutoa maoni juu ya maslahi mapana ya Marekani katika Greenland.
Rais wa Ufaransa Emmanuel Macron (Kulia) akikutana na Rais mteule wa Marekani Donald Trump katika Ikulu ya Elysee mjini Paris, Ufaransa, Desemba 7, 2024. (Xinhua/Gao Jing)
Hata hivyo, baba yake, Trump, ameonyesha maoni tofauti wakati akirejelea safari hiyo kwenye mtandao wake wa kijamii wa Truth Social. "Don Jr. na wawakilishi wangu wakitua Greenland. Mapokezi yamekuwa mazuri. Wao, na Dunia Huria, wanahitaji usalama, ulinzi na AMANI! Hili ni jambo ambalo lazima litokee. MAGA. MAKE GREENLAND GREAT AGAIN!" ameandika.
Greenland, eneo linalojitawala ndani ya Ufalme wa Denmark, ilipata mamlala ya ndani ya kujitawala mwaka 1979 na kupanua serikali yake yenyewe mwaka 2009.
people.cn © Tovuti ya Gazeti la Umma