Lugha Nyingine
Slovakia inaweza kusimamisha msaada kwa Ukraine kutokana na mzozo wa usafirishaji gesi: Waziri Mkuu Fico
Waziri Mkuu wa Slovakia Robert Fico (Kulia) akikutana na Kamishna wa Nishati wa Umoja wa Ulaya (EU) Dan Jorgensen mjini Brussels, Ubelgiji, Januari 9, 2025. (Umoja wa Ulaya/kupitia Xinhua)
BRUSSELS - Waziri Mkuu wa Slovakia Robert Fico amesema mjini Brussels kwamba serikali yake inafikiria kusimamisha msaada wa kibinadamu kwa Ukraine kama sehemu ya hatua za kukabiliana na mzozo unaoendelea wa usafirishaji gesi ya Russia.
Akizungumza na waandishi wa habari mjini Brussels jana Alhamisi baada ya kukutana na Kamishna wa Nishati wa Umoja wa Ulaya (EU) Dan Jorgensen, Fico amesema Slovakia inatathmini hatua zitakazochukuliwa, ikiwa ni pamoja na kupigia kura ya veto maamuzi ya EU kuhusiana na Ukraine. Hatua zingine ni pamoja na kukata njia za dharura za kusambaza umeme kwa Ukraine na kupunguza msaada kwa wakimbizi wa vita wa Ukraine.
Fico amesisitiza kuwa Slovakia haina lengo la kuzidisha mivutano bali itatekeleza hatua hizo kama hakuna suluhisho litakalofikiwa. Pia ametangaza kuanzishwa kwa kikundi kazi na Kamisheni ya Ulaya kushughulikia suala hilo.
Mzozo huo umezuka baada ya mkataba wa usafirishaji gesi kati ya Ukraine na Russia kumalizika Desemba 31 mwaka jana. Usafirishaji gesi huo hadi Slovakia ulikoma siku iliyofuata huku Rais wa Ukraine Volodymyr Zelensky akiamua kutohuisha makubaliano.
Kuhusu kusimamishwa kwa usafirishaji huo wa gesi kutoka Russia, Fico ameonya juu ya athari kubwa za kiuchumi, akikadiria hasara inayoweza kutokea yenye thamani ya euro karibu bilioni 1.5 (dola za Kimarekani kama bilioni 1.55) kwa Slovakia na euro bilioni karibu 70 kwa EU.
Waziri Mkuu wa Slovakia Robert Fico (wa kwanza, kushoto) akikutana na Kamishna wa Nishati wa Umoja wa Ulaya (EU) Dan Jorgensen mjini Brussels, Ubelgiji, Januari 9, 2025. (Umoja wa Ulaya/ kupitia Xinhua)
people.cn © Tovuti ya Gazeti la Umma