

Lugha Nyingine
Mjumbe Maalum wa Rais Xi Ashiriki Hafla ya Kuapishwa kwa Rais wa Venezuela
Rais wa Venezuela Nicolas Maduro (kulia) akikutana na mjumbe maalum wa Rais Xi Jinping wa China Wang Dongming, ambaye pia ni naibu mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge la Umma la China, huko Caracas, Venezuela, Januari 10, 2025. (Ikulu ya Venezuela/kupitia Xinhua)
CARACAS - Mjumbe Maalum wa Rais Xi Jinping wa China Wang Dongming, ambaye pia ni naibu mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge la Umma la China ameshiriki kwenye hafla ya kuapishwa kwa Rais wa Venezuela Nicolas Maduro kutokana na mwaliko wa serikali ya Venezuela siku ya Ijumaa, na amekutana na rais huyo katika ikulu yake mjini Caracas baada ya kuapishwa kwake.
Wang aliwasilisha salamu za kikunjufu za Rais Xi na za kutakia kila la kheri kwa Rais Maduro na kumpongeza kwa kuchaguliwa tena kuwa rais wa Venezuela.
Wang amesema, Septemba 2023, marais Xi na Maduro kwa pamoja walitangaza kuinua hadhi ya uhusiano kati ya China na Venezuela kuwa uhusiano wa wenzi wa ushirikiano wa kimkakati wa siku zote, ikipeleka uhusiano wa pande mbili katika zama mpya.
“Mwaka jana, pande hizo mbili zilisherehekea kwa taadhima maadhimisho ya miaka 50 tangu kuanzishwa kwa uhusiano wa kidiplomasia, na urafiki kati ya nchi hizo mbili umekita mizizi zaidi katika mioyo ya watu wa nchi hizo mbili,” Wang amesema.
Ameeleza kuwa China ina nia ya kushirikiana na Venezuela katika kuendelea kutekeleza maoni muhimu yaliyofikiwa na wakuu wa nchi hizo mbili, kuimarisha na kuendeleza urafiki wa jadi, na kusukuma mbele uhusiano wa pande mbili kwa manufaa ya watu wa nchi hizo mbili.
Kwa upande wake Rais Maduro amemwomba Wang kuwasilisha heshima yake ya juu na salamu za dhati kwa Rais Xi, na kutoa shukrani zake kwa Rais Xi kwa kutuma mjumbe maalum kushiriki kwenye hafla ya kuapishwa kwa awamu yake mpya.
Rais Maduro amesema, “Venezuela inaweka umuhimu mkubwa sana kuendeleza uhusiano wa wenzi wa ushirikiano wa kimkakati wa siku zote kati ya China na Venezuela, na inaiunga mkono kithabiti China katika kulinda maslahi yake makuu,” Venezuela inapenda kushirikiana na China katika kuhimiza ushirikiano wenye manufaa halisi katika sekta mbalimbali, kuimarisha mawasiliano ya kubadilishana maoni kuhusu uzoefu wa utawala wa nchi, na kuhimiza uhusiano wa pande mbili uendelezwe kwenye ngazi mpya.
people.cn © Tovuti ya Gazeti la Umma