

Lugha Nyingine
Rais wa Maldives akutana na Waziri wa Mambo ya Nje wa China
![]() |
Rais wa Maldives Mohamed Muizzu akikutana na Waziri wa Mambo ya Nje wa China Wang Yi, ambaye pia ni mjumbe wa Ofisi ya Siasa ya Kamati Kuu ya Chama cha Kikomunisti cha China (CPC), nchini Maldives, Januari 10, 2025. (Xinhua/Che Hongliang) |
MALE - Rais Mohamed Muizzu wa Maldives amekutana na Waziri wa Mambo ya Nje wa China Wang Yi siku ya Ijumaa, huku pande zote mbili zikiapa kuzidisha ushirikiano wa pande mbili katika maeneo mbalimbali wakati Wang alipopita kwa muda mfupi nchini Maldives akirejea kutoka Afrika.
Muizzu amekumbushia ziara yake ya kiserikali yenye mafanikio nchini China mwaka jana na kusema nchi hizo mbili daima zimekuwa zikitendeana kwa uelewano na udhati.
Pande hizo mbili zimedumisha mawasiliano ya karibu ya ngazi ya juu na kupata matokeo makubwa katika ushirikiano, amesema rais huyo, akiongeza kuwa anafurahi kuona kwamba China imekuwa chanzo kikubwa cha watalii kusafiri nchini Maldives.
“Maldives inapenda kuwa mshirika wa karibu zaidi wa China, kuboresha urafiki wao wa jadi, kuimarisha ushirikiano katika nyanja mbalimbali, na kusukuma mbele uhusiano wa pande mbili kupata maendeleo makubwa zaidi” amesema rais Muizzu.
Rais Muizzu amesema Maldives inathamini kazi ya China katika kulinda amani na utulivu wa dunia na inapenda kuimarisha uratibu na ushirikiano na China katika masuala ya kimataifa na kikanda ili kulinda kwa pamoja haki na usawa wa kimataifa.
Kwa upande wake, Wang, ambaye pia ni mjumbe wa Ofisi ya Siasa ya Kamati Kuu ya Chama cha Kikomunisti cha China (CPC) amesema kuwa ziara yenye mafanikio ya Muizzu nchini China ilikuwa ni wakati muhimu katika uhusiano kati ya China na Maldives.
Amesema, katika ziara hiyo mwaka jana, wakuu wa nchi hizo mbili walikubaliana kupandisha uhusiano wa pande mbili kwenye ushirikiano wa kimkakati na wa kiwenzi wa pande zote na kudhamiria kujenga kwa pamoja jumuiya ya China na Maldives yenye mustakabali wa pamoja, ambayo imeweka mustakabali ya uhusiano wa pande mbili.
“Ushirikiano kati ya China na Maldives umeweka mfano mzuri wa kuheshimiana, kutendeana kwa usawa na maendeleo ya pamoja kati ya nchi kubwa na ndogo. China inamshukuru rais na serikali ya Maldives kwa kutekeleza kithabiti sera ya urafiki kwa China na kushikilia kanuni ya kuwepo kwa China moja.” Wang amesema.
Amesema, China, kama ilivyo muda wote, itaiunga mkono Maldives katika kulinda uhuru na mamlaka yake ya kitaifa na kutafuta njia ya maendeleo inayoendana na hali yake halisi ya kitaifa.
people.cn © Tovuti ya Gazeti la Umma