China inapinga vikali vizuizi vya Marekani kwa mauzo ya nje ya AI: Wizara ya Biashara

(Tovuti ya Gazeti la Umma) Januari 14, 2025

BEIJING - Wizara ya Biashara ya China imesema kuwa China inapinga vikali serikali ya Biden kutangaza vizuizi vya uuzaji nje wa bidhaa zinazohusiana na Akili Bandia (AI).

“Vizuizi hivyo vinaimarisha zaidi udhibiti wa uuzaji nje wa chipu za AI na vigezo vya modeli, huku vikipanua mamlaka ya nje ya Marekani. Vinaleta vikwazo na uingiliaji kwa pande za tatu zinazofanya biashara ya kawaida na China,” msemaji wa wizara hiyo amesema jana Jumatatu.

Amesema, hapo awali, kampuni za teknolojia ya hali ya juu na mashirika ya mambo ya AI ya Marekani yalionyesha kutoridhika na kueleza wasiwasi wao kupitia njia mbalimbali, yakisema kuwa hatua hizo za vizuizi zimeanzishwa kwa pupa bila kujadiliwa kwa kutosha na zinajumuisha udhibiti wa kupita kiasi wa sekta ya AI.

Msemaji huyo ameongeza kuwa, wadau hao wa Marekani kwa kuamini kuwa hatua hizo zitasababisha athari mbaya, wamehimiza sana serikali ya Biden kusitisha utekelezaji wake.

“Hata hivyo, serikali ya Biden imepuuza malalamiko ya wadau hao na kutaka kutekeleza mapema hatua hizi. Kitendo hiki ni mfano wa ujumlishaji wa dhana ya usalama wa taifa na matumizi mabaya ya udhibiti wa mauzo ya nje, ikiashiria ukiukaji wa wazi wa sheria za kimataifa za biashara ya pande nyingi,” msemaji huyo amesema.

Amesisitiza kuwa, kitendo hiki kimezuia sana biashara ya kawaida kati ya nchi mbalimbali, kudhoofisha sheria za soko na utaratibu wa uchumi wa kimataifa, na kuathiri uvumbuzi wa teknolojia duniani.

“Pia kimeharibu maslahi ya kampuni duniani kote, ikiwa ni pamoja na zile za Marekani” msemaji huyo amesema, akiongeza kuwa China itachukua hatua hitajika ili kulinda kithabiti haki na maslahi yake halali.

(Wahariri wa tovuti:Zhou Linjia,Zhao Jian)

Picha