

Lugha Nyingine
Watu 92,000 wawekwa chini ya kuwahamishwa kutokana na moto wa nyika wa Los Angeles, Marekani
Ndege ya kuzima moto ikidondosha dawa za kuzima moto ili kuzuia moto wa nyika usienee zaidi kwenye vilima vya Mandeville Canyon mjini Los Angeles, California, Marekani, Januari 11, 2025. (Picha na Qiu Chen/Xinhua)
LOS ANGELES - Mkuu wa Polisi Kaunti ya Los Angeles Robert Luna amewaambia waandishi wa habari jana Jumatatu kwamba, Watu takriban 92,000 wanaendelea kuwa chini ya amri ya lazima ya kuhamishwa kutokana na moto wa nyika wa Los Angeles magharibi mwa Marekani, na wengine 89,000 wako chini ya tahadhari ya kuhamishwa.
Watu takriban 25 wamefariki na wengine zaidi ya kumi na wawili hawajulikani waliko huku moto huo wa nyika ukizidi kushika kasi katika eneo la Los Angeles.
Moto huo mkali katika Kaunti ya Los Angeles, uliochochewa na hali mbaya ya ukame na upepo mkali, umeteketeza eneo lenye ukubwa wa ekari zaidi ya 40,500, na kuharibu majengo zaidi ya 12,300 mpaka jana Jumatatu.
Moto wa Palisades, ambao ndiyo mkubwa zaidi, ulikuwa umedhibitiwa kwa asilimia 14, na Moto wa Eaton, wa pili kwa ukubwa, ulikuwa umedhibitiwa kwa asilimia 33 mpaka Jumatatu asubuhi, Idara ya Misitu na Ulinzi wa Moto ya California (Cal Fire) imeeleza.
Wateja zaidi ya 80,000 katika jimbo hilo la California hawana huduma ya umeme wakati ambapo Kampuni ya Umeme ya Southern California Edison ikianza kuzima umeme katika sehemu za Kusini mwa California kabla ya tukio lijalo la upepo, ambalo lilitabiriwa kuanza leo Jumanne, kwa saa za huko.
people.cn © Tovuti ya Gazeti la Umma