UN: Mwitikio wa msaada waongezeka kwa waathiriwa wa Kimbunga cha Dikeledi Kusini Mashariki mwa Afrika

(CRI Online) Januari 14, 2025

Wadau wa Umoja wa Mataifa wanakabiliana na Kimbunga cha Kitropiki cha Dikeledi kinacholikumba eneo la kusini mashariki mwa Afrika, kikiwa na upepo mkali na mvua kubwa.

Ofisi ya uratibu wa misaada ya kibinadamu ya Umoja wa Mataifa (OCHA) imesema wadau wa Umoja wa Mataifa wameanza kufanya kazi na mamlaka za ndani baada ya kimbunga hicho kulikumba eneo la kaskazini mwa Madagascar, lililokumbwa na kimbunga kikali cha Chido karibu mwezi mmoja uliopita.

Tahadhari ya hivi karibuni ya OCHA imesema kiini cha kimbunga cha Dikeledi kiko kwenye bahari ya Msumbiji, umbali wa kilomita takriban 75 kutoka pwani ya jimbo la Nampula kaskazini mashariki mwa Msumbiji.

Serikali ya Madagascar imeripoti kuwa watu watatu wamefariki na wengine zaidi ya 350 wamekimbia makazi yao, zaidi ya watu 5,200 wameathirika moja kwa moja, karibu nyumba 1,300 zimefurika maji, na vituo vitano vya afya vimebomolewa.

(Wahariri wa tovuti:Song Ge,Zhao Jian)

Picha