

Lugha Nyingine
Biashara na uwekezaji wa kuvuka mpaka wa China waimarika zaidi
Picha ikionyesha mwonekano wa Bandari ya Tangshan katika Mkoa wa Hebei, kaskazini mwa China, Januari 13, 2025. (Picha na Liu Mancang/Xinhua)
BEIJING - Biashara na uwekezaji wa kuvuka mpaka wa China uliimarika zaidi mwaka 2024, amesema Li Bin, naibu mkuu wa Mamlaka ya Ubadilishanaji Fedha za Kigeni (SAFE) ya Serikali ya China akinukuu takwimu rasmi siku ya Jumanne kwenye mkutano na waandishi wa habari ulioandaliwa na Ofisi ya Habari ya Baraza la Serikali ya China.
Amesema, mapato na malipo ya kuvuka mipaka ya sekta zisizo za kibenki, ikiwa ni pamoja na kampuni na watu binafsi, yaliongezeka kwa asilimia 14.6 na kufikia dola za Kimarekani trilioni 14.3 mwaka jana, yakifikia rekodi ya juu.
“Usawa wa kimsingi ulidumishwa kati ya mapato na malipo, na akiba ya fedha za kigeni ilikuwa zaidi ya dola za Kimarekani trilioni 3.2,” Li amesema, akiongeza kuwa kiwango cha ubadilishaji cha RMB na fedha za kigeni kilitulia kwa ujumla katika kiwango mwafaka na chenye uwiano.
Ameongeza kuwa mali za mambo ya kifedha nje ya nchi ilizidi trilioni 10 kwa mara ya kwanza mwishoni mwa Septemba mwaka 2024.
Akibainisha kuwa sera za uchumi mkuu za China zitasaidia kuimarisha juhudi katika marekebisho ya kukabiliana na mzunguko wa kiuchumi, Li amesema idara ya SAFE itatekeleza sera zenye ufanisi zaidi za usimamizi wa ubadilishaji fedha za kigeni ili kuunga mkono maendeleo yenye sifa bora ya uchumi na ufunguaji mlango wa kiwango cha juu.
Akizungumza kwenye mkutano huo na waandishi wa habari, Xuan Changneng, naibu mkuu wa Benki ya Kuu ya China (PBOC), amesema kuwa mwaka 2024, benki hiyo ilitekeleza hatua nne muhimu za marekebisho ya sera ya mambo ya fedha yenye lengo la kudumisha ufufukaji wa uchumi na kuunga mkono maendeleo yenye sifa bora ya uchumi.
“Hatua hizo ni pamoja na kupunguza kiwango cha akiba ya fedha kwa jumla ya asilimia 1 na kiwango cha riba cha benki kuu kwa jumla ya asilimia 0.3,” Xuan ameeleza.
Amesema, mwaka 2024, sera ya mambo ya fedha ya China imepata matokeo mazuri, huku kukiwa na ukuaji mwafaka katika kiwango cha jumla cha fedha.
people.cn © Tovuti ya Gazeti la Umma