

Lugha Nyingine
Uchumi wa mji mkuu wa China, Beijing waongezeka kwa asilimia 5.2 mwaka 2024
Picha hii iliyopigwa Septemba 2, 2024 ikionyesha mwonekano wa maghorofa ya eneo kuu la biashara (CBD) majira ya jioni mjini Beijing, mji mkuu wa China. (Xinhua/Wang Jianhua)
BEIJING - Pato la Jumla (GDP) la mji mkuu wa China, Beijing, limeongezeka karibu asilimia 5.2 mwaka 2024, meya wa mji huo Yin Yong amesema Jumanne wakati akitoa ripoti ya kazi ya serikali kwenye mkutano wa mwaka wa Bunge la Umma la Mji wa Beijing, akiongeza kuwa Pato la Jumla kwa kila mtu limeendelea kuwa la juu zaidi nchini kote.
“Huku kukiwa na changamoto nyingi na kukabiliana na mazingira magumu, mji wa Beijing umetekeleza hatua mbalimbali mahsusi ili kuhakikisha ukuaji thabiti na mzuri wa uchumi wa jumla wa mji huo," Yin amesema.
Mwaka jana, Beijing iliimarisha na kuboresha sekta za viwanda vya hali ya juu ambazo ni injini yake ya uchumi, kwa kutekeleza sera 40 mahsusi za kuunga mkono viwanda kama vile vifaa tiba na nyenzo mpya.
Mafanikio ya Beijing katika sekta hizo za teknolojia ya hali ya juu yamejikita sana katika mtandao wake mkubwa wa uvumbuzi, haswa katika vituo muhimu kama Zhongguancun, ambayo inajulikana kama "Bonde la Silicon" nchini China.
Kwa kuendana na mwelekeo mpana wa kitaifa wa kuchochea ukuaji wa uchumi, mji huo ulianzisha sera mbalimbali ya soko la nyumba, ambayo ilijumuisha kupunguza viwango vya malipo na viwango vya rehani na kupunguza vizuizi kwa manunuzi, hali ambayo ilihimiza kutuliza na kufufua soko la nyumba.
"Soko la nyumba katika miji mikubwa kama Beijing linaonyesha dalili wazi za kutulia, huku wakazi wakipata imani tena katika kununua nyumba," amesema Gao Yuan, mkurugenzi wa Taasisi ya Utafiti ya Kampuni wakala wa nyumba ya Beijing Lianjia.
Beijing pia ilishuhudia kustawi kwa usafiri wa kitalii mwaka 2024, ukitoa mchango mkubwa katika hali yake ya kiuchumi. Jumla ya abiria katika viwanja vya ndege viwili vya mji huo ilizidi milioni 117, ikiwa ni ongezeko la asilimia 26.2 mwaka hadi mwaka, huku wasafiri wa kimataifa wakichukua asilimia 16.8 ya jumla.
Idadi ya watalii wanaoingia Beijing iliongezeka kwa asilimia 186.8 ikilinganishwa na mwaka uliopita, ukiweka rekodi mpya za idadi ya watalii na mapato, ripoti hiyo imeeleza.
Kwa kuangalia mipango ya mbele mwaka 2025, Yin ameonyesha kuwa Beijing inalenga ukuaji wa Pato la Jumla wa asilimia takriban 5, ikiendeleza mwelekeo wake wa upigaji hatua thabiti huku kukiwa na utulivu.
people.cn © Tovuti ya Gazeti la Umma