

Lugha Nyingine
Serikali ya Marekani yaiondoa Cuba kwenye orodha ya nchi mfadhili wa ugaidi
Rais Joe Biden wa Marekani akizungumza katika Ikulu ya Marekani White House mjini Washington, D.C., Marekani, Januari 5, 2025. (Xinhua/ Yousong)
WASHINGTON - Rais wa Marekani Joe Biden ameliarifu Bunge siku ya Jumanne kwamba serikali yake itaondoa Cuba kutoka kwenye orodha ya nchi mfadhili wa ugaidi, Ikulu ya Marekani White House imesema, ikiwa ni sehemu ya makubaliano ya kuachilia wafungwa wa kisiasa katika nchi hiyo na wale wanaochukuliwa na Marekani kuwa wamewekwa vizuizini kinyume cha haki na serikali hiyo mjini Havana.
Maafisa waandamizi wa serikali ya Biden walioelezea uamuzi huo wa rais kwa waandishi wa habari wamesema kwamba hatua hiyo imechukuliwa baada ya serikali kukamilisha tathmini na kuhitimisha "hakuna ushahidi wa kuaminika" unaoonyesha kuwa Cuba kwa sasa inaunga mkono ugaidi wa kimataifa.
Kwa kufanya hivyo, Rais Biden amebatilisha uamuzi wa Rais wa zamani Donald Trump, alioufanya Januari mwaka 2021 wa kuiorodhesha tena Cuba katika orodha ya nchi mfadhili wa ugaidi.
Rais Trump alifanya hivyo katika siku za mwisho za muhula wake wa kwanza wa urais ili kubatilisha juhudi za kutafuta maafikiano na Cuba zilizoanzishwa na Rais wa zamani Barack Obama, ambaye katika muhula wake wa pili madarakani Marekani iliondoa uamuzi huo.
Maafisa waandamizi hao wa serikali ya Biden wanatarajia Cuba itawaachilia "makumi kadhaa" ya wafungwa wakati ambapo Trump atakuwa ameshaapishwa tena kuwa rais Januari 20.
Pia siku ya Jumanne, Biden alitia saini waraka wa kumbukumby ya usalama wa taifa wa kubatilisha sera ya vikwazo dhidi ya Cuba ya mwaka 2017 ya Rais wa wakati huo Trump inayojulikana kama "Waraka wa 5 wa Kumbukumbu ya Rais ya Usalama wa Taifa," ikihitimisha mara moja vikwazo kwa watu na taasisi fulani za Cuba zinazofanya biashara ya kifedha na watu na taasisi za Marekani.
Ili kuhimiza zaidi serikali ya Cuba kuachilia wafungwa hao, serikali ya Biden umetoa msamaha kwa Ibara ya III ya Sheria ya Helms Burton kwa muda wa miezi sita, kwa mujibu wa taarifa ya msemaji wa ikulu ya Marekani White House Karine Jean-Pierre.
Hatua hiyo, kwa hiyo, itazuia raia wa Marekani au watu wengine kuwasilisha madai katika mahakama za Marekani kuhusu mali iliyotwaliwa na serikali ya Cuba baada ya Mapinduzi ya Cuba ya mwaka 1959.
Maafisa waadanmizi hao na Jean-Pierre pia wamedokeza kwenye mchango wa makubaliano ya kuachiliwa kwa wafungwa hao wa Cuba kutoka kwa Kanisa Katoliki linaloongozwa na Papa Francis, ambaye Rais Biden alimtunuku Nishani ya Rais ya Uhuru siku ya Jumamosi wiki iliyopita.
people.cn © Tovuti ya Gazeti la Umma