WFP: Watu laki mbili wamekimbia mapigano mashariki mwa DRC

(CRI Online) Januari 16, 2025

Shirika la Mpango wa Chakula Duniani (WFP) limesema takriban watu laki mbili wamekimbia makazi yao kwenye eneo la mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) kutokana na mapigano makali kati ya jeshi la nchi hiyo na makundi yenye silaha tangu mwezi Novemba mwaka jana.

WFP imesema mapigano hayo, yanayohusisha waasi wa kundi la M23 na makundi mengine ambayo yalikiuka makubaliano ya usimamishaji vita yaliyoanzia Agosti 4 mwaka 2024, mpaka sasa yamelazimu watu wapatao laki mbili kukimbia makwao katika Jimbo la Kivu Kaskazini na majimbo mengine nchini DRC.

Shirika hilo limeonya kuwa hali ya kibinadamu nchini humo haswa katika eneo la mashariki inaendelea kuzorota wakati mapigano hayo yakipamba moto.

Majumuisho ya hivi karibuni ya hali halisi yanaonyesha kuwa takriban watu milioni 25.6 nchini DRC wanakabiliwa na ukosefu wa usalama wa chakula.

(Wahariri wa tovuti:Zhou Linjia,Zhao Jian)

Picha