

Lugha Nyingine
Daniel Chapo aapishwa kuwa Rais wa Msumbiji
Rais mpya wa Msumbiji Daniel Francisco Chapo akionyesha ishara ya mamlaka aliyopokea kutoka kwa Lucia Ribeiro, Mwenyekiti wa Baraza la Katiba la nchi hiyo, kwenye hafla ya kuapishwa kwake mjini Maputo, Msumbiji, Januari 15, 2025. (AIM/kupitia Xinhua)
MAPUTO - Daniel Francisco Chapo ameapishwa kuwa rais wa awamu ya tano wa Msumbiji kwenye hafla ya hadhara iliyofanyika Jumatano katikati mwa Maputo, mji mkuu wa nchi hiyo ya kusini mwa Afrika.
“Kwa mujibu wa Ibara ya 149, aya ya 1, ya Katiba, namtangaza Mheshimiwa Daniel Francisco Chapo kuapishwa kuwa Rais wa Jamhuri ya Msumbiji,” ametangaza Lucia Ribeiro, mwenyekiti wa Baraza la Katiba la nchi hiyo.
Hafla hiyo iliyofanyika katika Uwanja wa Uhuru ilihudhuriwa na watu mashuhuri, wakiwemo marais wa zamani Joaquim Chissano na Armando Guebuza, vilevile mkuu wa nchi anayemaliza muda wake Filipe Nyusi.
Rais wa Afrika Kusini Cyril Ramaphosa na Rais wa Guinea-Bissau Umaro Sissoco Embalo pia walihudhuria hafla hiyo, pamoja na wageni wengine zaidi ya 2,000, wakiwemo wawakilishi wa serikali, mashirika, washirika wa ushirikiano na viongozi wengine mashuhuri.
Katika hotuba yake ya kuapishwa, Chapo ametangaza mipango kwa ajili ya mageuzi ya kiutawala, ikiwa ni pamoja na kupunguza idadi ya wizara na kuondoa nyadhifa kama vile manaibu waziri, kupeleka rasilimali kwenye sekta muhimu. "Itakuwa serikali ndogo zaidi, lakini ni yenye unyumbufu na fanisi wa hali ya juu," amesema.
Nafasi ya naibu waziri itawekewa mbadala wa “makatibu wa nchi wenye majukumu ya wazi na yaliyoainishwa vyema, ambao wanawajibika moja kwa moja kwa mawaziri,” amesema Chapo.
Amechukua msimamo mkali dhidi ya rushwa na kuahidi kupitia marupurupu wanayopewa viongozi wa serikali na kubinafsisha kampuni zisizo za kimkakati ili kuifanya serikali iwe endelevu zaidi.
Chapo pia amesisitiza dhamira ya utawala wake katika kukabiliana na utekaji nyara na uhalifu wa kupangwa.
Akihitimisha hafla hiyo, Rais anayemaliza muda wake Filipe Nyusi ametoa wito wa kuwepo kwa umoja miongoni mwa raia wa Msumbiji katika kumuunga mkono krais mpya. "Ninawaomba wananchi wote wa Msumbiji kushikamana kumwunga mkono Rais Daniel Chapo, ili aweze kuongoza nchi kwa njia bora iwezekanavyo," Nyusi amesema.
Akiwa ni Katibu Mkuu wa sasa wa chama tawala cha Frelimo, Daniel Chapo alizaliwa katika jimbo la kati la Sofala mwaka 1977 na kuhitimu Shahada ya Sheria katika Chuo Kikuu cha Eduardo Mondlane mwaka 2000, ikimfanya kuwa Rais wa kwanza wa Jamhuri aliyezaliwa baada ya uhuru wa nchi hiyo mwaka 1975.
Desemba 23, 2024, Chapo alitangazwa na Baraza la Katiba kuwa rais mteule kwa kupata asilimia 65.17 ya kura zote halali zilizopigwa katika uchaguzi mkuu wa tarehe 9 Oktoba.
people.cn © Tovuti ya Gazeti la Umma