

Lugha Nyingine
Makamu Rais wa China ashiriki kwenye hafla ya kuapishwa kwa Rais Trump
Makamu Rais wa China Han Zheng akiwa mjumbe maalum wa Rais Xi Jinping wa China, amekutana na Makamu Rais mteule wa Marekani J.D. Vance mjini Washington, D.C., Marekani, Januari 19, 2025. (Xinhua/Liu Weibing)
WASHINGTON – Kutokana na mwaliko, Makamu Rais wa China Han Zheng, ambaye pia ni mjumbe maalum wa Rais wa China Xi Jinping ameshiriki kwenye hafla ya kuapishwa kwa Rais wa Marekani Donald Trump Jumatatu mjini Washington, D.C. ambapo akiwa nchini humo, amekutana na Makamu Rais mteule wa Marekani J.D. Vance, wajumbe wa sekta za viwanda na biashara wa Marekani, Ofisa Mtendaji Mkuu wa Tesla Elon Musk, Mwenyekiti Mstaafu wa Taasisi ya Brookings ya Marekani, John Thornton na wengine.
Kwenye mkutano wake na Vance siku ya Jumapili, Han kwanza aliwasilisha salamu za Rais Xi kwa Rais Trump na kumpongeza Vance kwa kuchaguliwa kwake.
Han amesema kuwa hivi karibuni Rais Xi alikuwa na mazungumzo muhimu na Trump kwa njia ya simu, ambapo viongozi hao wawili wamefikia maoni mengi muhimu ya pamoja kuhusu maendeleo ya uhusiano kati ya China na Marekani katika kipindi kijacho.
“China inapenda kushirikiana na Marekani katika kushikilia uelekezaji wa kimkakati wa diplomasia ya mkuu wa nchi na kutekeleza maoni muhimu ya pamoja yaliyofikiwa kati ya marais Xi na Trump, ili kusukuma mbele maendeleo tulivu, mazuri na endelevu ya uhusiano wa pande mbili”, Han amesema.
Kwa upande wake, Vance amemuomba Han kuwasilisha salamu za dhati za Rais Trump kwa Rais Xi.
Vance amesema Rais Trump alikuwa na mazungumzo na Rais Xi kwa njia ya simu siku chache zilizopita, ambapo walikuwa na mawasiliano mazuri kuhusu masuala muhimu kuhusu uhusiano wa pande mbili. Amesisitiza kuwa uhusiano wa kiuchumi na kibiashara ni muhimu kwa nchi mbili Marekani na China.
Alipokutana na wajumbe wa sekta za viwanda na biashara wa Marekani, Han amesema, mwanzo mzuri na maendeleo tulivu ya uhusiano kati ya China na Marekani vinalingana na ustawi wa pamoja wa watu wa nchi mbili China na Marekani na matarajio ya pamoja ya jumuiya ya kimataifa.
“China itaendeleza kithabiti mageuzi na ufunguaji mlango, na kuendelea kuboresha na kurahisisha mazingira ya biashara,” ameongeza.
Katika mikutano yake na Musk na Thornton, Han amekaribisha kampuni na sekta mbalimbali za Marekani kutumia fursa, na kufanya juhudi zaidi za kufaidika pamoja na matunda ya maendeleo ya China.
Ametoa wito wa kuhimiza mawasiliano na ushirikiano kati ya pande mbili katika sekta mbalimbali za uchumi, biashara na utamaduni, na kuongeza maelewano na urafiki kati ya watu wa pande hizo mbili, ili kuendelea kuboresha na kuimarisha siku hadi siku msingi wa nia ya umma kwa uhusiano kati ya China na Marekani.
people.cn © Tovuti ya Gazeti la Umma