

Lugha Nyingine
Trump aapishwa kuwa rais wa 47 wa Marekani
Watu wakitazama matangazo moja kwa moja ya hafla ya kuapishwa kwa rais wa 47 wa Marekani kwenye Ukumbi wa Capital One mjini Washington, D.C., Marekani, Januari 20, 2025. (Xinhua/Wu Xiaoling)
WASHINGTON - Donald Trump ameapishwa kuwa rais wa 47 wa Marekani katika Ukumbi wa Rotunda wa Bunge la Marekani, akianza muhula wake wa pili, huku akirejea Ikulu ya Marekani baada ya miaka minne, ambapo kutokana na utabiri wa hali ya hewa ya baridi mjini Washington, D.C., hafla hiyo imefanyika eneo la ndani – ikiwa ni mara ya kwanza katika miongo minne iliyopita.
Trump amekula kiapo chake cha kushika madaraka kilichoongozwa na Jaji Mkuu wa Marekani, John Roberts. Jaji Mkuu kwa kawaida husimamia kiapo cha rais kuingia madarakani, desturi ambayo imefuatwa tangu hafla ya kwanza ya uapisho.
Trump amesema katika hotuba yake ya kuapishwa kuwa kudidimia kwa Marekani kumeisha na "Zama ya dhahabu ya Marekani inaanza hivi sasa."
Kwenye hotuba yake hiyo, Trump ameahidi kutia saini "maagizo kadhaa za kiutawala ya kihistoria," ikiwa ni pamoja na kutangaza dharura ya kitaifa katika mpaka wa kusini, kuimarisha uzalishaji wa mafuta na gesi, kuondoa sera nafuu kwa magari yanayotumia umeme. Pia ameahidi kuanza mara moja marekebisho ya mfumo wa biashara na kutoza "ushuru kwa nchi za nje."
Trump ameahidi kupunguza bei, kuokoa sekta ya magari, "kurejesha mfumo wa sheria wenye haki, usawa na bila upendeleo," na kurejesha sheria na utaratibu katika miji nchini Marekani.
Akikosoa mipango ya chama cha Democrat za DEI (Uanuwai, Usawa na Ujumuishaji), rais huyo mpya amesema wiki hii, pia atakomesha sera ya serikali ya "kujaribu kuingiza mambo ya rangi na jinsia katika kila nyanja ya maisha ya umma na ya kibinafsi," na "kuunda jamii isiyojali rangi za watu na vigezo vya uwezo na sifa."
Trump pia ameahidi kujenga jeshi imara zaidi kuwahi kuonekana duniani. "Tutapima mafanikio yetu, si tu kwa vita tunavyoshinda, lakini pia kwa vita ambavyo tunamaliza na labda muhimu zaidi, vita ambavyo hatutashiriki," Trump amesema, akiongeza kuwa atakuwa mjenga amani na muunganishaji.
Amebainisha kuwa itakuwa "sera rasmi" ya serikali ya Marekani kwamba kuna jinsia mbili tu -- kiume na kike.
Rais huyo amesisitiza kwamba atabadilisha jina la Ghuba ya Mexico kuwa Ghuba ya Marekani, na atarudisha Mfereji wa Panama kwa Marekani.
Aidha, Trump amesema kuwa, kwa mara ya pili, ataiondoa Marekani kutoka kwenye Mkataba wa Paris juu ya mabadiliko ya tabianchi.
Muda mfupi kabla ya kuapishwa kwa Trump, JD Vance aliapishwa kuwa makamu wa rais wa Marekani.
people.cn © Tovuti ya Gazeti la Umma