Mkutano wa WEF watoa wito wa ushirikiano wa kimataifa, ukionya vizuizi vya biashara havitumikii maslahi ya yeyote

(Tovuti ya Gazeti la Umma) Januari 24, 2025

Picha hii iliyopigwa Januari 20, 2025 ikionyesha nembo ya Baraza la Uchumi Duniani (WEF) mjini Davos, Uswizi. (Xinhua/Lian Yi)

Picha hii iliyopigwa Januari 20, 2025 ikionyesha nembo ya Baraza la Uchumi Duniani (WEF) mjini Davos, Uswizi. (Xinhua/Lian Yi)

DAVOS, Uswisi - Huku kukiwa na hali ya kutokuwa na uhakika na kuongezeka kwa kujihami kiuchumi duniani ambako hakujawahi kushuhudiwa, mkutano wa mwaka wa Baraza la Uchumi Duniani (WEF) umesisitiza haja ya dharura ya kuwepo kwa uchumi wa dunia ulio wazi, jumuishi na kuimarishwa kwa ushirikiano wa kimataifa ili kushughulikia changamoto za kiuchumi na kuhakikisha ufufukaji endelevu.

Ufufukaji dhaifu wa uchumi

Uchumi wa dunia unaelekea katika mwaka mwingine wa hali ya kutokuwa na uhakika na ukuaji usio na uwiano, kwa mujibu wa ripoti mpya ya Mtazamo wa Wachumi Wakuu wa WEF, ambayo imezinduliwa kabla ya mkutano huo wa mwaka wenye kaulimbiu ya "Ushirikiano kwa Zama za Teknolojia za Kisasa" mwaka huu.

Mtazamo huo unasema asilimia 56 ya wachumi wakuu hao waliohojiwa wanatarajia uchumi wa dunia kudhoofika mwaka 2025, ikilinganishwa na asilimia 17 pekee wanaokadiria kuboreshwa. Aidha, mijadala muhimu katika mkutano huo wa mwaka ilitawaliwa na maneno kama vile "hali ya kutokuwa na uhakika kwa kiwango cha juu" na "katika njia panda."

Shirika la Fedha la Kimataifa (IMF) lilitoa ripoti mpya kuhusu mtazamo wake wa kimataifa Januari 17, likikadiria ukuaji wa uchumi wa dunia kwa asilimia 3.3 mwaka 2025 na 2026. Hata hivyo, takwimu hiyo iko chini ya wastani wa kiwango cha ukuaji wa mwaka wa asilimia 3.7 kutoka mwaka 2000 hadi 2019.

Watu wakihudhuria Baraza la Uchumi Duniani (WEF) mjini Davos, Uswizi, Januari 20, 2025. (Xinhua/Lian Yi)

Watu wakihudhuria Baraza la Uchumi Duniani (WEF) mjini Davos, Uswizi, Januari 20, 2025. (Xinhua/Lian Yi)

Suluhu ya Dunia kwa Matatizo ya Dunia

Kuongezeka kwa migogoro ya siasa za kijiografia na kukosekana kwa utulivu wa kikanda vimeleta kiwango cha ushirikiano wa kimataifa kwenye kiwango cha chini, kwa mujibu wa ripoti ya Kipimajoto cha Ushirikiano Duniani Mwaka 2025 iliyotolewa na WEF Januari 7.

Akizungumza katika mkutano huo wa mwaka wa WEF siku ya Jumanne, Rais wa Kamisheni ya Ulaya Ursula von der Leyen amebainisha kuwa dunia imeingia katika zama mpya ya ushindani mkali wa kimkakati wa kijiografia. "Tutahitaji kushirikiana ili kuepusha mashindano ya kimataifa hadi chini kwa sababu haiko katika maslahi ya yeyote kuvunja dhamana katika uchumi wa dunia," amesema.

Huku akitambua hali ya sasa ya ushindani na mielekeo ya kulinda maslahi ya ndani katika nchi nyingi, Rais wa WEF Borge Brende amesisitiza kuwa ushirikiano unaendelea kuwa njia pekee ya kutatua changamoto za pamoja duniani.

Biashara Huria, Hakuna Kujihami

Kujihami kiuchumi kumeibuka kuwa jambo la kutiliwa wasiwasi sana katika mkutano huo. Ripoti hiyo ya Mtazamo wa Wachumi Wakuu wa WEF imeonya kuwa kuongezeka kwa vizuizi vya biashara na migogoro ya siasa za kijiografia kunaweza kusababisha migogoro ya kudumu ya mifumo ya biashara.

Zaidi ya nusu ya wachumi waliohojiwa wanaona mustakabali mbaya unaochochewa na vizuizi vya kibiashara, kuongezeka kwa deni la umma, na ufufukaji wa uchumi usioendana kwa usawa duniani.

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres akizungumza kwenye Mkutano wa Mwaka wa Baraza la Uchumi Duniani mjini Davos, Uswizi, Januari 22, 2025. (Xinhua/Lian Yi)

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres akizungumza kwenye Mkutano wa Mwaka wa Baraza la Uchumi Duniani mjini Davos, Uswizi, Januari 22, 2025. (Xinhua/Lian Yi)

IMF pia imeonya dhidi ya hatua za upande mmoja kama vile ushuru, vizuizi visivyo vya kiushuru au ruzuku ambazo zinaweza kuumiza washirika wa biashara na kuchochea kulipiza kisasi.

Brende ameonya kuwa kutengana kiuchumi na kibiashara kunaweza kuwa na athari mbaya kwa uchumi wa dunia.

IMF inakadiria kuwa kutengana vikali, pamoja na ushuru wa juu, vinaweza kupunguza uchumi wa dunia kwa asilimia 7.

(Wahariri wa tovuti:Zhou Linjia,Zhao Jian)

Picha