Wamisri waandamana karibu na kivuko cha mpakani cha Rafah dhidi ya uhamishaji wa Wapalestina kutoka Gaza

(Tovuti ya Gazeti la Umma) Februari 01, 2025

Watu wakiandamana kupinga kuhamishwa kwa Wapalestina kutoka kwenye ardhi yao kwenye upande wa Misri wa kivuko cha mpakani cha Rafah, Januari 31, 2025. (Xinhua/Str)

Watu wakiandamana kupinga kuhamishwa kwa Wapalestina kutoka kwenye ardhi yao kwenye upande wa Misri wa kivuko cha mpakani cha Rafah, Januari 31, 2025. (Xinhua/Str)

CAIRO - Maelfu ya watu wameandamana jana Ijumaa karibu na upande wa Misri wa kivuko cha mpakani cha Rafah, kituo pekee kinachounganisha Misri na Ukanda wa Gaza, kuelezea upinzani wao dhidi ya Wapalestina kuhamishwa kutoka Ukanda wa Gaza kupelekwa maeneo mengine.

Kituo cha kitaifa cha Televisheni cha Nile cha Misri kimeonyesha waandamanaji hao wakipeperusha bendera za Misri na Palestina na kupeperusha mabango yanayosomeka "hakuna kuhamishwa."

Waandamanaji hao walijumuisha viongozi wa kisiasa kutoka bunge la Misri na raia ambao walipiga kelele za kukataa wito wa kuhamisha Wapalestina kutoka kwenye ardhi yao kwenda Misri na Jordan.

Siku ya Alhamisi, Rais wa Marekani Donald Trump alisisitiza kuwa Misri na Jordan zitakubaliana na pendekezo lake la kuhamisha Wapalestina kutoka Gaza kwenda nchi hizo mbili, ambalo limeleta mabishano.

"Watafanya hivyo... Tunafanya mengi kwa ajili yao, na watafanya hivyo," Trump aliwaambia waandishi wa habari alipoulizwa kama atafikiria kuchukua hatua za kuishinikiza Cairo na Amman kukubali mpango wake huo.

Siku ya Jumatano, Rais wa Misri Abdel-Fattah al-Sisi alisema kuwa kuhamishwa kwa Wapalestina ni kitendo cha "udhalimu," ambacho Misri haitakishiriki. 

(Wahariri wa tovuti:Song Ge,Zhao Jian)

Picha