

Lugha Nyingine
China yawasilisha malalamiko kwa WTO dhidi ya Marekani kuongeza ushuru
BEIJING - China imewasilisha malalamiko kwenye utaratibu wa kutatua migogoro wa Shirika la Biashara Duniani (WTO) dhidi ya uamuzi wa Marekani wa kutoza ushuru wa asilimia 10 zaidi kwa bidhaa kutoka China, Wizara ya Biashara ya China (MOC) imesema.
Hatua hiyo ni kulinda haki na maslahi halali ya China, amesema msemaji wa wizara hiyo wakati akijibu maswali kutoka kwa waandishi wa habari siku ya Jumanne.
“Hatua ya Marekani ya kutoza ushuru zaidi kwa bidhaa za China umekiuka sana sheria za WTO, na kitendo hiki kibaya ni mfano wazi wa uendeshaji mambo kwa maslahi ya upande mmoja na kujihami kibiashara,” amesema msemaji huyo.
Msemaji huyo amesema hatua hiyo ya Marekani inadhoofisha kwa kiasi kikubwa mfumo wa biashara wa pande nyingi unaozingatia sheria, inabomoa msingi wa ushirikiano wa kiuchumi na kibiashara kati ya China na Marekani, na kuvuruga utulivu wa minyororo ya kimataifa ya uzalishaji na usambazaji.
Marekani kwa kujirudia imekukuwa ikiweka maslahi ya upande mmoja juu ya yale ya pande nyingi, ikisababisha shutuma kali kutoka kwa pande wanachama wengi wa WTO, amesema msemaji huyo, akiongeza kuwa "China inapinga vikali hatua hizo za Marekani, na inaitaka Marekani irekebishe mara moja makosa yake."
“China ikiwa ni nchi inayounga mkono na inayotoa mchango mkubwa mfumo wa biashara wa pande nyingi, inapenda kushirikiana na pande wanachama wengine wa WTO kushughulikia changamoto zinazoletwa na maslahi ya upande mmoja na kujihami kibiashara kwenye mfumo wa biashara wa pande nyingi, na kulinda maendeleo yenye utaratibu na tulivu ya biashara ya kimataifa” ameongeza msemaji huyo.
people.cn © Tovuti ya Gazeti la Umma