

Lugha Nyingine
Rais wa Afrika Kusini akanusha tuhuma za Trump za "kunyang’anya ardhi" dhidi yake
Picha iliyopigwa Machi 7, 2023 ikionyesha mawio ya jua mjini Johannesburg, Afrika Kusini. (Picha na Shiraaz Mohamed/Xinhua)
JOHANNESBURG - Rais Cyril Ramaphosa wa Afrika Kusini amekanusha kauli husika zilizotolewa na Rais wa Marekani Donald Trump hivi karibuni kwamba "Afrika Kusini inapora ardhi, na inawatendea watu wa tabaka fulani VIBAYA SANA", akisisitiza kuwa nchi yake "haijapora ardhi."
Katika taarifa iliyotolewa na Ikulu ya Afrika Kusini, serikali ya nchi hiyo pia imetupilia mbali madai kwamba Sheria ya Kutwaa Ardhi imelenga kupora ardhi.
"Sheria ya Kutwaa Ardhi iliyopitishwa hivi karibuni si chombo cha kupora ardhi, bali ni mchakato wa kisheria ulioidhinishwa kikatiba ambao unahakikisha upatikanaji wa ardhi kwa umma kwa njia ya usawa na haki kama inavyoelekezwa na Katiba," imesema taarifa hiyo.
Jibu hilo la Ramaphosa limefuatia ujumbe wa Trump kwenye mtandao wake wa kijamii wa Truth Social siku ya Jumapili. "Afrika Kusini inapora ardhi, na inawatendea watu wa tabaka fulani VIBAYA SANA. Nitakata ufadhili wote wa siku zijazo kwa Afrika Kusini hadi uchunguzi kamili wa hali hii ukamilike," Trump aliandika.
Rais Ramaphosa amesema kwamba anatarajia kufanya majadiliano na Trump kuhusu mchakato wa mageuzi ya ardhi ya Afrika Kusini, akiashiria kwamba wanaweza kupata maafikiano. "Tunatazamia kuzungumza na serikali ya Trump kuhusu sera yetu ya mageuzi ya ardhi na masuala yenye maslahi ya pande mbili," Ramaphosa amesema.
Picha iliyopigwa Machi 7, 2023 ikionyesha mawio ya jua mjini Johannesburg, Afrika Kusini. (Picha na Shiraaz Mohamed/Xinhua)
Waziri wa Uhusiano na Ushirikiano wa Kimataifa wa Afrika Kusini, Ronald Lamola amesema hakuna jambo la kipekee kuhusu Sheria ya Kutwaa Ardhi, kwani nchi kama Marekani na Uingereza zina sheria zinazofanana ambazo zinaruhusu kuchukua ardhi wakati inapokuwa ni kwa maslahi ya umma.
Wakati huo huo, Msemaji wa Chama tawala cha ANC, Mahlengi Bhengu-Motsiri amekaribisha mazungumzo ya Rais Ramaphosa na marais wa kigeni.
"Chama cha ANC hakitavumilia upotoshaji wa ukweli unaodhoofisha mamlaka yetu na ajenda ya mageuzi. Tunatoa wito kwa makundi yote ya upigaji hatua, ndani na nje ya nchi, kukataa ajenda ya mgawanyiko ya AfriForum na kusimama na Afrika Kusini katika kutafuta kwake haki, usawa, na mageuzi ya ardhi yenye maana," amesema.
Mwezi Januari, Rais Ramaphosa alitia saini Mswada wa Sheria ya Kutwaa Ardhi, ambao unaruhusu taasisi za umma kuchukua ardhi kwa maslahi ya umma. Kutiwa saini kwa Sheria hiyo kulifuta Sheria ya mwaka 1975 kabla ya Afrika Kusini kuwa nchi ya kidemokrasia.
people.cn © Tovuti ya Gazeti la Umma