Mashirika ya kibinadamu ya UN yaonesha wasiwasi kuhusu kuongezeka kwa uhasama nchini Sudan

(CRI Online) Februari 05, 2025

Mashirika ya Umoja wa Mataifa nchini Sudan yameonesha wasiwasi kufuatia kuongezeka kwa vitendo vya uhasama katika Jimbo la Darfur Kaskazini na Kordofan Kusini kunakosababisha ongezeko la vifo vya raia na watu waliokimbia makazi yao.

Shirika la Kimataifa la Uhamiaji (IOM), limesema katika kipindi cha miezi 10 iliyopita, zaidi ya watu laki 6 walikimbia mji wa El Fasher na maeneo mengine ya Darfur Kaskazini ili kutafuta usalama.

Ofisi ya uratibu wa masuala ya kibinadamu ya Umoja wa Mataifa (OCHA) imesema katika wiki za hivi karibuni, mashambulizi yameripotiwa katika mji wa El Fasher na maeneo ya jirani, ikiwa ni pamoja na kambi ya Abu Shouk, hospitali ya Saudi na maeneo ya magharibi ya mji huo.

OCHA pia imesema inasikitishwa na kuongezeka kwa vitendo vya uhasama huko Kordofan Kusini, huku kukiwa na mapigano kati ya jeshi la Sudan na Kundi la harakati ya ukombozi wa Sudan tawi la Kaskazini (SPLM-N).

Ofisi hiyo imesema zaidi ya watu milioni 13 nchini Sudan wanahitaji misaada ili kukabiliana na matishio ya milipuko, lakini ufadhili wa kukabiliana na matishio hayo bado ni mdogo.

(Wahariri wa tovuti:Song Ge,Zhao Jian)

Picha