Nchi za Mashariki ya Kati zalaani pendekezo la Marekani la kuhamisha Wapalestina kutoka Gaza

(Tovuti ya Gazeti la Umma) Februari 06, 2025

Watoto wa Palestina wakionekana karibu na hema ambalo hutumika kama makazi ya muda kwenye uwanja wa michezo wa Al-Yarmouk katika Jiji la Gaza, Februari 5, 2025. (Picha na Rizek Abdeljawad/Xinhua)

Watoto wa Palestina wakionekana karibu na hema ambalo hutumika kama makazi ya muda kwenye uwanja wa michezo wa Al-Yarmouk katika Jiji la Gaza, Februari 5, 2025. (Picha na Rizek Abdeljawad/Xinhua)

CAIRO – Serikali za nchi za Mashariki ya Kati na viongozi wa kikanda wameeleza kukataa pendekezo la Rais wa Marekani Donald Trump siku ya Jumatano kwamba Washington inaweza kuchukua udhibiti wa Gaza na kuhamisha Wapalestina, wakilielezea pendekezo hilo kuwa ni uvunjaji wa sheria ya kimataifa na tishio kwa juhudi za muda mrefu za kufikia suluhu ya mataifa mawili.

Trump alidokeza wazo hilo kwenye mkutano na waandishi wa habari wa pamoja na Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu siku ya Jumanne, akisema kwamba Marekani "itatwaa Ukanda wa Gaza" na kuuendeleza upya, ingawa hakutoa maelezo mahsusi juu ya kuwahamishia kwenye makazi mapya Wapalestina.

"Tutakwenda kuuendeleza, kutengeneza maelfu ya ajira, na litakuwa jambo ambalo Mashariki ya Kati nzima itaweza kujivunia," alisema.

Katika taarifa yake, Jumuiya ya Nchi za Kiarabu (AL) imekataa pendekezo hilo la Trump, ikisema linakiuka sheria ya kimataifa na kutishia utulivu wa kikanda. AL imesisitiza tena kwamba suala la Palestina linaendelea kuwa chini ya makubaliano ya Waarabu, ikisisitiza kwamba moja ya kanuni zake muhimu ni kuhakikisha haki halali ya watu wa Palestina ya kuanzisha nchi huru kwa kuzingatia mipaka ya mwaka 1967, huku Jerusalem Mashariki ikiwa mji wake mkuu.

Rais wa Marekani Donald Trump (Kulia) na Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu wakifanya mkutano wa pamoja na waandishi wa habari katika Ikulu ya White House mjini Washington D.C., Marekani, Februari 4, 2025. (Xinhua/Hu Yousong)

Waziri wa Mambo ya Nje wa Uturuki Hakan Fidan amelielezea pendekezo hilo la Gaza kuwa "halikubaliki" na kimsingi lina dosari. "Hata kuwazia mpango kama huo ni makosa," Fidan ameliambia shirika la habari la Anadolu katika mahojiano.

Fidan pia amesisitiza msimamo thabiti wa Uturuki kuhusu haki za Wapalestina, akikataa juhudi zozote za kuiondoa Hamas katika ujenzi upya na utawala wa Gaza.

Wizara ya Mambo ya Nje ya Saudi Arabia imetoa taarifa siku hiyo ya Jumatano, ikisisitiza kwamba msimamo wa Saudi Arabia kuhusu kuanzishwa kwa taifa la Palestina ni usio na mjadala.

"Nchi itaendelea na juhudi zake za dhati za kuanzisha taifa huru la Palestina huku Jerusalem Mashariki ikiwa mji wake mkuu na haitaanzisha uhusiano wa kidiplomasia na Israel bila hilo," taarifa hiyo imesema.

Kwenye mkutano uliofanyika mjini Cairo, Waziri wa Mambo ya Nje wa Misri, Badr Abdelatty na Waziri Mkuu wa Palestina aliyekuwa ziarani mjini Cairo, Mohammad Mustafa, wamehimiza kuendelea kwa juhudi za kuirejesha Gaza bila kulazimisha Wapalestina kuondoka katika ukanda huo, hasa kwa wale bado wana dhamira ya kubaki.

Mtoto wa Palestina akionekana juu ya jengo lililobomolewa kwenye kambi ya wakimbizi ya Jabalia kaskazini mwa Ukanda wa Gaza, Januari 29, 2025. (Picha na Abdul Rahman Salama/Xinhua)

Mtoto wa Palestina akionekana juu ya jengo lililobomolewa kwenye kambi ya wakimbizi ya Jabalia kaskazini mwa Ukanda wa Gaza, Januari 29, 2025. (Picha na Abdul Rahman Salama/Xinhua)

Mfalme wa Jordan Abdullah II, kwenye mkutano wake na Rais wa Palestina Mahmoud Abbas huko Amman, pia amekataa majaribio yoyote ya kunyakua ardhi au kuwaondoa Wapalestina.

"Tunasisitiza tena umuhimu wa kupatikana kwa haki na amani ya pande zote kwa kuzingatia suluhu ya mataifa mawili, ambayo itapelekea kuanzishwa kwa taifa huru la Palestina huku Jerusalem Mashariki ikiwa mji wake mkuu, kwa kuzingatia mipaka ya mwaka 1967," taarifa hiyo kutoka Kasri la Kifalme la Hashemite la Jordan imesema.

Umoja wa Falme za Kiarabu (UAE) pia imetangaza siku hiyo ya Jumatano kukataa vikali wazo la kuhamisha Wapalestina kwa nguvu.

Majengo yaliyobomolewa yakionekana kwenye kambi ya wakimbizi ya Jabalia kaskazini mwa Ukanda wa Gaza, Januari 29, 2025. (Picha na Abdul Rahman Salama/Xinhua)

Majengo yaliyobomolewa yakionekana kwenye kambi ya wakimbizi ya Jabalia kaskazini mwa Ukanda wa Gaza, Januari 29, 2025. (Picha na Abdul Rahman Salama/Xinhua)

(Wahariri wa tovuti:Song Ge,Zhao Jian)

Picha