

Lugha Nyingine
Marekani haiwezi kujitoa kutoka kwenye chombo ambacho Marekani si sehemu yake tena: UNHRC
Wajumbe wakihudhuria kikao cha mkutano wa 56 wa Baraza la Haki za Kibinadamu la Umoja wa Mataifa mjini Geneva, Uswisi, Juni 18, 2024. (Xinhua/Lian Yi)
GENEVA - Baraza la Haki za Kibinadamu la Umoja wa Mataifa (UNHRC) limesema jana Alhamisi kwamba hadi kufikia Januari 1, 2025, muda wa Marekani kuwa nchi mwanachama ulikuwa umeshaisha, ikiifanya isiwe na haki ya kujitoa kutoka kwenye chombo hicho cha kati ya serikali mbalimbali ambacho haikuwa sehemu yake tena.
"Kwa rekodi, Marekani ilikuwa nchi mwanachama wa Baraza la Haki za Kibinadamu kuanzia Januari 1, 2022, hadi Desemba 31, 2024. Tangu Januari 1, 2025, Marekani si nchi mwanachama tena wa Baraza la Haki za Kibinadamu na ikawa nchi mwangalizi, kama ilivyo kwa nchi 193 wanachama wa Umoja wa Mataifa ambazo si wanachama wa Baraza," Pascal Sim msemaji wa UNHRC amesema katika taarifa yake kwa Shirika la Habari la China, Xinhua.
Ameongeza kuwa, nchi mwenye hadhi ya uangalizi wa Baraza hilo haiwezi kujitoa kutoka kwenye chombo hicho ambacho nchi hiyo si sehemu yake tena.
Picha hii iliyopigwa tarehe 29 Februari 2024 ikionyesha mwonekano wa nje wa Ofisi ya Umoja wa Mataifa (UN) mjini Geneva, Uswisi. (Xinhua/Shi Song)
“Kama sehemu ya kanuni, na katika moyo wa majadiliano ya pande nyingi ambao ni sifa ya Baraza, tunakaribisha na kuhimiza kushiriki kwa kila Nchi Mwanachama wa Umoja wa Mataifa - iwe kama nchi mwanachama au nchi mwangalizi wa Baraza - katika kazi ya Baraza na mfumokazi wake," taarifa hiyo imeongeza.
Rais wa Marekani Donald Trump siku ya Jumanne alitia saini amri ya utendaji, kuitoa Marekani kutoka UNHRC.
UNHRC inaundwa na nchi wanachama 47, huku theluthi takriban moja ya nafasi zake zikichaguliwa kila mwaka. Nchi wanachama hutumikia mihula ya miaka mitatu na zinaweza kuchaguliwa tena kwa mara moja.
Wakati wa muhula wa kwanza wa Trump, Marekani ilijitoa kutoka UNHRC mwezi Juni 2018. Mwezi Februari 2021, Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani wakati huo Antony Blinken alitangaza kwamba utawala wa Joe Biden utashiriki tena kwenye Baraza hilo kama nchi mwangalizi. Marekani ilirejea kwenye baraza hilo mwezi Januari 2022 kama nchi mwanachama kamili.
Picha hii iliyopigwa Mei 22, 2024 ikionyesha Ikulu ya White House mjini Washington, D.C., Marekani. (Xinhua/Liu Jie)
people.cn © Tovuti ya Gazeti la Umma