Benki Kuu ya Uganda yapoteza Shilingi Bilioni 62

(CRI Online) Februari 07, 2025

Polisi nchini Uganda imethibitisha kuwashikilia maafisa tisa wa Wizara ya Fedha ya nchi hiyo kwa uchunguzi wa tuhuma za kudukua mifumo ya benki kuu na kuiba kiasi cha shilingi za Uganda bilioni 62 (dola za Kimarekani kama milioni 16.87).

Hii ni baada ya wizi mkubwa kutokea Novemba mwaka jana, ambapo Waziri wa Fedha wa Uganda, Henry Musasizi, alithibitisha kuwa akaunti za Benki Kuu ya Uganda zilidukuliwa na fedha kuhamishwa kinyume cha sheria.

Polisi imesema kuwa maafisa hao, wakiwemo kutoka idara ya hazina na ofisi ya mhasibu mkuu wa wizara, wanashikiliwa kwa ajili ya kusaidia uchunguzi wa tukio hilo.

Wadukuzi hao, wakijitambulisha kwa jina la “Taka”, walifanikiwa kudukua mifumo ya TEHAMA ya Benki Kuu ya Uganda na kuhamisha kiasi hicho cha fedha kwa njia haramu.

(Wahariri wa tovuti:Song Ge,Zhao Jian)

Picha