

Lugha Nyingine
Botswana kushughulikia hali duni ya elimu katika maeneo ya vijijini na pembezoni
Waziri wa Ustawi wa Watoto na Elimu ya Msingi wa Botswana Nono Mokoka (Kulia) akitoa taarifa kwa wanahabari juu ya matokeo ya Mtihani wa Cheti kwa Wanafunzi wa Elimu ya Msingi (JCE) mjini Gaborone, Botswana, Februari 6, 2025. (Picha na Tshekiso Tebalo/Xinhua)
GABORONE - Botswana imepanga kutenga rasilimali zaidi kwa shule za vijijini ili kuziba pengo la elimu kati ya wanafunzi wa vijijini na mijini kufuatia kutolewa kwa matokeo ya hivi karibuni ya Mtihani wa Cheti kwa Wanafunzi wa Elimu ya Msingi (JCE).
Akizungumza kwenye mkutano na wanahabari juu ya matokeo hayo ya JCE mjini Gaborone siku ya Alhamisi, Waziri wa Ustawi wa Watoto na Elimu ya Msingi wa Botswana Nono Mokoka amesema ujenzi wa miundombinu umepewa kipaumbele cha juu cha serikali. "Hakuna namna tunaweza kuzungumzia shule rafiki kwa watoto bila ya kuwa na miundombinu stahiki."
Matokeo hayo ya JCE kimsingi hutumika kwa wanafunzi kuingia shule za sekondari, huku wanafunzi jumla ya 45,284 wakifanya mtihani. Kwa ujumla kiwango cha kufaulu katika shule za serikali uliimarika kidogo, huku asilimia ya wanafunzi waliopata daraja C au bora (daraja la ufaulu) ikipanda kwa asilimia 1.46, kutoka asilimia 37.10 hadi asilimia 38.57. Asilimia ya wanafunzi waliopata daraja la E au bora zaidi iliongezeka kwa asilimia 2.44 kutoka asilimia 83.10 hadi asilimia 85.54.
Licha ya mafanikio hayo Mokoka amesema kuwa shule za serikali bado ziko nyuma ya shule za binafsi. Pia ameeleza wasiwasi wake kuwa wanafunzi 11,526 wamepata daraja la chini au la X, huku mikoa yenye kiwango cha chini zaidi cha kufaulu ikiwa ni Ghanzi na Kaskazini Magharibi, yote iko vijijini.
Amesisitiza umuhimu wa usawa na msawazisho wa huduma, akisema kuwa wanafunzi wa maeneo ya vijijini na wale walio katika mazingira magumu zaidi wanapaswa kupewa kipaumbele na kupewa rasilimali sawa na wenzao wa mijini ili kuhakikisha ushindani wa haki.
"Tutajikita katika kuunga mkono wanafunzi katika maeneo ya pembezoni na walio katika mazingira magumu zaidi ili kuwasaidia kufanikiwa," amesema.
people.cn © Tovuti ya Gazeti la Umma