

Lugha Nyingine
Misri kuandaa mkutano wa dharura wa wakuu wa Nchi za Kiarabu kuhusu suala la Palestina
Wapalestina wakionekana kwenye mtaa wenye majengo yaliyobomolewa katika kambi ya wakimbizi ya Jabalia kaskazini mwa Ukanda wa Gaza, Januari 29, 2025. (Picha na Abdul Rahman Salama/Xinhua)
CAIRO - Misri imetangaza kwamba Cairo itakuwa mwenyeji wa mkutano wa dharura wa wakuu wa nchi za Kiarabu Tarehe 27 mwezi huu wa Februari ili kushughulikia matukio ya siku hizi kuhusu suala la Palestina na Ukanda wa Gaza, Wizara ya Mambo ya Nje ya Misri imesema katika taarifa yake ya Jumapili.
Taarifa hiyo imeeleza kuwa, mkutano huo imeamuliwa ufanyike baada ya mashauriano ya ngazi ya juu kati ya Misri na nchi za Kiarabu, ikiwa ni pamoja na Palestina, ambayo iliomba kuitisha mkutano huo, na uratibu na Bahrain, mwenyekiti wa sasa wa mkutano wa viongozi wa Jumuiya ya Nchi za Kiarabu (AL) na sekretarieti ya AL.
Taarifa hiyo inafuatia maneno yenye utata aliyosema Rais wa Marekani Donald Trump ya kupendekeza kuhamishwa kwa Wapalestina kutoka Gaza hadi nchi jirani, zikiwemo Misri na Jordan. Pendekezo hilo limekataliwa na watu wengi wa pande zote za kikanda na kimataifa.
Kwenye mkutano wa pamoja na waandishi wa habari mjini Washington na Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu siku ya Jumanne wiki iliyopita, Rais Trump alisema kuwa Marekani inapanga kuchukua udhibiti wa Ukanda wa Gaza na kuuendeleza upya baada ya kuhamisha wakaazi wake Wapalestina.
Trump hapo awali aliwahi kudokeza mapendekezo kama hayo, ambayo zote Misri na Jordan zimeyakataa waziwazi, zikisisitiza tena kupinga kuwalazimisha Wapalestina kufanya uhamishaji wowote.
people.cn © Tovuti ya Gazeti la Umma