Mashirka ya Waafrikaner nchini Afrika Kusini yakataa pendekezo la Trump la kuwapa makazi mapya

(Tovuti ya Gazeti la Umma) Februari 10, 2025

JOHANNESBURG - Mashirika yanayowakilisha watu wa Jamii ya Waafrikaner nchini Afrika Kusini yakiwemo yale ya Solidarity na AfriForum yamesema kuwa hayatakubali ombi la Rais wa Marekani Donald Trump la kuwapa makazi mapya nchini Marekani.

Mashirika hayo yalifanya mkutano na wanahabari siku ya Jumamosi mjini Pretoria kujibu mwito wa Trump uliotolewa Ijumaa, ambayo imeishutumu Afrika Kusini kwa "kupora mali ya wakulima wa Waafrikaner," na kuwapa Waafrikaner fursa ya kutafuta hadhi ya ukimbizi nchini Marekani.

Kwenye mahojiano kwa njia ya simu siku ya Jumapili, Kallie Kriel, afisa mtendaji mkuu wa shirika la kizengezi la jamii hiyo ya Waafrikaner, AfriForum, ameliambia Shirika la Habari la China, Xinhua kwamba wawakilishi wa jamii hiyo ya Waafrikaner watasafiri kwenda Marekani kukutana na utawala wa Trump baadaye mwezi huu.

Alipoulizwa kuhusu madai ya "kupora ardhi kimabavu," Kriel amesema hali hiyo ilitokea lakini haikufanywa na serikali.

"Kupora ardhi kimabavu kunafanywa na watu wanaochochewa kisiasa. Sababu ya serikali kulaumiwa ni kwamba hawachukulii hili kwa uzito au kulizuia," Kriel amesema.

Siku ya Jumamosi, Idara ya Uhusiano na Ushirikiano wa Kimataifa ya Afrika Kusini (DIRCO) ilieleza wasiwasi wake juu ya mwito wa Trump wa kukata msaada wa kifedha kwa nchi hiyo.

Marekani ilitenga dola karibu milioni 440 za Kimarekani katika msaada kwa Afrika Kusini mwaka 2023, kwa mujibu wa ripoti za vyombo vya habari vya Marekani.

Mvutano kati ya nchi hizo mbili ulianza mapema wiki iliyopita wakati Trump alipotishia kuondoa ufadhili wake kwa Afrika Kusini kutokana na Sheria ya kutwaa Ardhi iliyotiwa saini hivi karibuni, ambayo inaruhusu taasisi za umma kuchukua ardhi kwa maslahi ya umma.

"Inatia wasiwasi mkubwa kwamba msingi wa mwito huo hauna usahihi wa ukweli na unashindwa kutambua historia ya kina na chungu ya Afrika Kusini ya ukoloni na ubaguzi wa rangi," DIRCO imesema katika taarifa.

Taarifa hiyo pia imeelezea kama "kichekesho" kwamba serikali ya Marekani inatoa hifadhi ya ukimbizi kwa watu wa jamii ya Waafrikaner "wenye upendeleo zaidi wa kiuchumi" katika nchi yao wakati huo huo ikiwafukuza watu wanaotafuta hifadhi kutoka nchi nyingine.

(Wahariri wa tovuti:Zhou Linjia,Zhao Jian)

Picha