

Lugha Nyingine
Israel yatoa amri ya utayari wa kijeshi baada ya Hamas kusema kuahirisha kuachilia huru mateka
Jamaa za mateka aliyeachiliwa huru wakikumbatiana wakati helikopta iliyombeba mateka huyo ilipowasili katika kituo cha matibabu mjini Ramat Gan, Israel, Februari 8, 2025. (Picha na Gil Cohen Magen/Xinhua)
JERUSALEM/GAZA - Israel imetoa amri ya jeshi kuwa tayari kwa "hali yoyote inayoweza kutokea katika Ukanda wa Gaza" baada ya Hamas kutangaza jana Jumatatu katika taarifa yake kwamba makabidhiano ya mateka yaliyopangwa Jumamosi yataahirishwa hadi kutolewa kwa uarifu mwingine, na katika taarifa iliyotolewa na ofisi yake, Waziri wa Ulinzi wa Israel Israel Katz amelaani taarifa ya Hamas kuwa "imekiuka kabisa makubaliano ya kusimamisha mapigano Gaza na kuachilia huru mateka."
Katz amesema ameamuru Vikosi vya Ulinzi vya Israeli "kujiandaa kwa ngazi ya juu zaidi kwa hali yoyote wezekana huko Gaza na kulinda jamii zilizo karibu na ukanda huo."
Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu alikuwa akiongoza mkutano wa kutathmini hali na mawaziri na maofisa wa usalama, tovuti ya habari ya Ynet ya Israel imeripoti, ikiinukuu Ofisi ya Waziri Mkuu.
Watu wakimkaribisha mfungwa wa Palestina aliyeachiliwa huru katika mji wa Ramallah, Kando ya Magharibi, Februari 8, 2025. (Picha na Ayman Nobani/Xinhua)
Mapema siku hiyo ya Jumatatu, Abu Obeida, msemaji wa Brigedi za Al-Qassam, tawi la kijeshi la Hamas, alisema katika taarifa yake kwamba katika muda wa wiki tatu zilizopita, viongozi wa vuguvugu la kupinga uvamizi wa Israel wamekuwa wakifuatilia kushindwa kwa Israel kufuata masharti ya makubaliano ya kusimamisha mapigano.
Mapungufu hayo ni pamoja na kuahirisha kurejea kwa watu waliokimbia makazi yao kaskazini mwa Gaza na kuwalenga kwa makombora na risasi, vilevile kutoleta misaada kwa aina zake zote kama ilivyokubaliwa, taarifa hiyo iliongeza, ikisisitiza vuguvugu hilo la upinzani limetekeleza majukumu yake yote.
“Kwa maana hiyo, makabidhiano ya mateka yataahirishwa hadi kutolewa kwa uarifu mwingine na hadi Israeli ihakikishe inafuata makubaliano na kufidia kwa wiki zilizopita kurudi nyuma."
"Tutafuata ahadi yetu kwa masharti ya makubaliano wakati wakaliaji watakapotoa ahadi yao" amesema msemaji huyo.
Wapalestina waliokimbia makazi yao ambao wanarejea nyumbani kutoka kusini mwa Ukanda wa Gaza kuelekea kaskazini, wakionekana karibu na Ushoroba wa Netzarim katikati mwa Ukanda wa Gaza, Februari 9, 2025. (Picha na Rizek Abdeljawad/Xinhua)
Wakati huo huo, Kurugenzi ya Mateka, Watu Waliopotea, na Wanaorejea ya Israel, ambayo ni chombo cha serikali, imesema katika taarifa kwamba Israel "inasisitiza juu ya utekelezaji kamili wa makubaliano kama yalivyoandikwa na inafuatilia kwa umakini ukiukaji wowote juu ya makubaliano."
Hatua hizo zinajiri saa chache baada ya wajumbe wa Israel kurejea kutoka Qatar, ambako mazungumzo yasiyo ya moja kwa moja yalifanyika kuhusu makubaliano ya kipindi kijacho ya kusimamisha mapigano kati ya Israel na Hamas.
Chini ya makubaliano ya sasa ya usimamishaji vita, ambayo yalianza kutekelezwa Januari 19 baada ya miezi 15 ya vita, mateka 21 -- Waisraeli 16 na Wathailand watano -- wameachiliwa kutoka Gaza kwa mabadilishano ya mamia ya wafungwa wa Palestina walioachiliwa kutoka jela za Israel.
Katika makubaliano hayo ya kipindi cha kwanza cha muda wa wiki sita, mateka 33 wa Israel na wafungwa wapatao 2,000 wa Palestina walikuwa wakitarajiwa kuachiliwa huru.
people.cn © Tovuti ya Gazeti la Umma