

Lugha Nyingine
Ushuru wa Marekani kwa chuma na aluminiamu wazua upingaji mkali kote Ulaya
Rais wa Kamisheni ya Ulaya Ursula von der Leyen akizungumza kwenye mkutano na waandishi wa habari baada ya mkutano wa kilele wa Baraza la Ulaya mjini Brussels, Ubelgiji, Desemba 19, 2024. (Xinhua/Zhao Dingzhe)
BRUSSELS - Uamuzi wa Rais wa Marekani Donald Trump wa kutoza ushuru wa asilimia 25 kwa bidhaa za chuma na aluminiamu zinazouzwa kwa Marekani, bila kujali nchi zilikotoka, umezua upingaji mkali kote Ulaya.
Rais wa Kamisheni ya Ulaya Ursula von der Leyen ameonya jana Jumanne kwamba ushuru huo wa Marekani kwa kuagiza chuma na aluminiamu kutoka Umoja wa Ulaya (EU) "utaanzisha hatua thabiti na sawia za kulipiza."
"Kutoza ushuru kwa bidhaa za EU bila msingi wowote hautapita bila kujibiwa," von der Leyen amesema katika taarifa. "EU itachukua hatua kulinda maslahi yake ya kiuchumi. Tutalinda wafanyakazi, wafanyabiashara na watumiaji wetu."
Akihutubia wajumbe wa Bunge la Ulaya (MEPs) mjini Strasbourg siku hiyo ya Jumanne, Kamishna wa Ulaya anayeshughulikia Mambo ya Biashara na Usalama wa Kiuchumi Maros Sefcovic amesema kuwa EU itajibu "kithabiti na sawia" kwa hatua hiyo ya Marekani.
Chansela wa Ujerumani Olaf Scholz amesisitiza tena msimamo wa Umoja wa Ulaya kuhusu hatua za kulipiza. "Kama Marekani itatuacha bila chaguo lingine, EU itajibu kwa msimamo mmoja," amesema katika hotuba yake kwa Bunge la Ujerumani, Bundestag siku hiyo ya Jumanne.
Hata hivyo, ameonya dhidi ya kuongezeka kwa mvutano. "Natumai tunaweza kuepuka njia potofu ya ushuru na ushuru wa kulipiza, kwani vita vya kibiashara hatimaye vitaharibu ustawi wa pande zote mbili," ameongeza.
Bendera za Umoja wa Ulaya zikipepea nje ya Jengo la Berlaymont, makao makuu ya Kamisheni ya Ulaya, mjini Brussels, Ubelgiji, Januari 29, 2025. (Xinhua/Meng Dingbo)
Waziri Mkuu wa Poland Donald Tusk amesema pia siku hiyo ya Jumanne kwamba Poland inajiandaa kwa ajili ya athari zitakazotokea kutokana na ushuru huo wa Marekani. "Inastahili kufanya kila kitu kuepusha vita visivyo vya lazima vya kibiashara na ushuru, kwa sababu hii inaleta matokeo mabaya kwa wazalishaji na watumiaji," Tusk amesema kabla ya mkutano wa serikali.
“Raundi hii mpya ya sera za kujihami kibiashara za Marekani inaweza kudhuru biashara ya kimataifa, kuvuruga minyororo ya usambazaji, na hatimaye kuelemea watumiaji nchini Marekani,” Fabrizio Hochschild, aliyekuwa naibu katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa, ameliambia Shirika la Habari la China, Xinhua.
Picha hii iliyopigwa Januari 20, 2023 ikionyesha Ikulu ya Marekani White House mjini Washington, D.C., Marekani. (Xinhua/Liu Jie)
"Historia inaonyesha kwamba maamuzi ya upande mmoja ya ushuru mara nyingi huchochea hatua za kulipiza kisasi, ikitatiza minyororo ya usambazaji na kudhoofisha utulivu wa kiuchumi," Hochschild amebainisha.
people.cn © Tovuti ya Gazeti la Umma