

Lugha Nyingine
IOM yatoa wito wa kuchangishwa dola milioni 81 kusaidia wahamiaji zaidi ya milioni 1.4 katika Pembe ya Afrika
Shirika la Kimataifa la Uhamiaji (IOM) na washirika wake 45 wa misaada ya kibinadamu na maendeleo Jumanne walitoa wito wa kuchangishwa dola milioni 81 za Marekani ili kutoa msaada wa kuokoa maisha kwa wahamiaji milioni 1.4 waliopo katika eneo la Pembe ya Afrika na Yemen mwaka 2025.
Ombi hilo la kuchangia fedha, ambalo lipo chini ya mpango wa kukabiliana na wahamiaji wa Pembe ya Afrika nchini Yemen na kusini mwa Afrika, linaloratibiwa na IOM pia litasaidia jamii zinazowahifadhi wahamiaji hao katika nchi za Djibouti, Ethiopia, Somalia, Tanzania, Kenya, na Yemen.
Katika taarifa aliyoitoa Nairobi, nchini Kenya, Mkurugenzi Mkuu wa IOM Amy Pope amesema bila ya uungwaji mkono wa haraka kwa wahamiaji na jamii zinazowahifadhi, mateso na mivutano itaongezeka, na misaada ya kuokoa maisha itaendelea kutopatikana.
Kwa mujibu wa IOM, mamia kwa maelfu ya wahamiaji hasa kutoka Ethiopia na Somalia hufunga safari za hatari, wakilenga kufika nchi za Ghuba zikiwemo Saudi Arabia kupitia Djibouti na Yemen. Pia husafiri kupitia Kenya, Tanzania na nchi nyingine za kusini mwa Afrika, wakitumai kufika Afrika Kusini.
people.cn © Tovuti ya Gazeti la Umma