

Lugha Nyingine
Msemaji: Utawala wa Taiwan unakosa udhati katika kurejesha utalii wa pande mbili za Mlango Bahari wa Taiwan
Zhu Fenglian, msemaji wa Ofisi ya Mambo ya Taiwan ya Baraza la Serikali la China akisema kwenye mkutano na waandishi wa habari mjini Beijing, Februari 12, 2025. (Xinhua/Chen Yehua)
BEIJING - Zhu Fenglian, msemaji wa Ofisi ya Mambo ya Taiwan ya Baraza la Serikali la China amekosoa utawala wa Chama cha Kidemokrasia cha Taiwan (DPP) kwa kutumia visingizio vya kiutaratibu kuahirisha urejeshaji tena wa utalii kati ya pande mbili za Mlango Bahari wa Taiwan.
“Utawala wa DPP umekuwa kikwazo kikuu cha urejeshaji tena wa utalii kati ya pande mbili za Mlango-Bahari, na si ukosefu wa mawasiliano kati ya mashirika ya utalii,” amesema Zhu kwenye mkutano na waandishi wa habari jana Jumatano.
Amesema, waendeshaji biashara ya utalii katika Mkoa wa Fujian na Mji wa Shanghai walikuwa wametuma maombi ya kutembelea kisiwa hicho, wakitarajia kufanya utafiti wa hali ya soko kwa urejeshaji tena wa safari za kwenda Taiwan kwa wakazi wa Fujian na Shanghai.
Ameeleza kwamba, Utawala wa DPP umedai kuwa mambo yanayohusu watalii wa China Bara kwenda Taiwan yanapaswa kujadiliwa kwanza kati ya Shirika la Utalii la Mlango Bahari wa Taiwan na Shirika la China Bara la Mawasiliano ya Utalii kati ya pande mbili za Mlango Bahari.
Zhu amesema China Bara haipingi mashirika hayo mawili kujadili mipango ya utalii wa pande mbili za Mlango Bahari baada ya urejeshaji wake tena.
"Kama Taiwan inadai iko tayari kukaribisha watalii wa China Bara, inapaswa kuruhusu ujumbe wa ukaguzi wa utalii kutembelea mara moja badala ya kutoa visingizio vya kuahirisha," Zhu amesema.
Amesema utawala wa DPP unakosa udhati katika urejeshaji tena wa utalii wa pande mbili za Mlango-Bahari na unatilia maanani zaidi ujanja wa kisiasa kuliko kuwezesha usafiri kwa watalii wa China Bara.
Aidha, Zhu amelaani ukataaji wa utawala wa DPP kutoa vibali vya kuingia kwa wajumbe wa Shanghai walioalikwa kushiriki katika Tamasha la Taa za Jadi la Taipei Mwaka 2025, akiielezea hali hiyo kuwa kitendo cha kizuizi cha kisiasa ambacho kinaharibu mawasiliano ya kitamaduni kati ya pande mbili za Mlango-Bahari.
Amezihimiza utawala wa DPP kuondoa vizuizi hivyo kwenye mawasiliano kati ya pande mbili za Mlango Bahari na kuchukua hatua za kivitendo kuruhusu watalii wa China Bara kutembelea.
people.cn © Tovuti ya Gazeti la Umma