

Lugha Nyingine
Ongezeko la idadi ya watu barani Afrika linahitaji hatua kali za usalama wa chakula
Wakati idadi ya watu barani Afrika ikitarajiwa kufikia bilioni 2.5 ifikapo mwaka 2050, bara hilo linapaswa kuimarisha uwezo wake endelevu wa uzalishaji na utengenezaji wa chakula ili kuhakikisha usalama wa chakula.
Wito huo umetolewa Alhamisi na Kamishna wa Umoja wa Afrika (AU) anayeshughulikia masuala ya kilimo, maendeleo ya vijijini, uchumi wa buluu na mazingira endelevu, Josefa Sacko, wakati alipokuwa akihutubia vyombo vya habari wakati wa kufanyika kwa Mkutano wa 38 wa Wakuu wa AU ambao umeanza Februari 12 na kuendelea hadi Februari 16 kwenye makao makuu ya AU huko Addis Ababa, Ethiopia.
Akibainisha athari mbaya za majanga ya kimataifa na kikanda, kuanzia changamoto za afya ya umma na milipuko hadi mgogoro unaoendelea nchini Ukraine pamoja na sintofahamu nyingine za siasa za kijiografia, Sacko alisema changamoto hizi zimechangiwa zaidi na kupanda kwa mfumuko wa bei, na kufanya usalama wa chakula kuwa suala muhimu zaidi.
Ameongeza kuwa mkakati wa Mpango Kabambe wa Maendeleo ya Kilimo wa Afrika wa miaka 10 na mpango kazi wa 2026-2035, uliopitishwa mapema mwaka huu, unatumika kama mwongozo wa kuendeleza maendeleo ya kilimo na mifumo ya chakula katika bara zima.
people.cn © Tovuti ya Gazeti la Umma