

Lugha Nyingine
Rais wa Angola amekuwa mwenyekiti wa zamu wa AU
Rais wa Angola Joao Lourenco akizungumza katika hotuba yake kwenye ufunguzi wa Mkutano wa 38 wa Kawaida wa Viongozi Wakuu wa Nchi na Serikali wa Umoja wa Afrika (AU) mjini Addis Ababa, Ethiopia, Februari 15, 2025. (Xinhua/Han Xu)
ADDIS ABABA - Rais wa Angola Joao Lourenco ameshika wadhifa wa mwenyekiti wa zamu wa Umoja wa Afrika (AU) kwenye ufunguzi wa Mkutano wa 38 wa Kawaida cha Baraza Kuu la Wakuu wa Nchi na Serikali wa AU huko Addis Ababa, Ethiopia huku Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa wa Djibouti Mahamoud Ali Youssouf akichaguliwa kuwa mwenyekiti mpya wa Kamati ya AU
Rais Lourenco amekuwa mwenyekiti wa AU badala ya Rais wa Mauritania Mohamed Ould Cheikh Ghazouani atakayeondoka kazini ambaye alishika wadhifa wa mwenyekiti wa jumuiya hiyo ya bara mwezi wa Februari mwaka jana kwenye mkutano wa 37 Baraza Kuu la AU.
Katika hotuba yake ya kukabidhiwa wadhifa huo, rais huyo wa Angola ameelezea dhamira yake kubwa ya kuharakisha matamanio makubwa ya Umoja wa Afrika kwa kupitia kuhimiza umoja wa bara na maendeleo ya jamii na uchumi .
“Kwa kufikiria siku za baadaye, matarajio yangu ni kukomesha migogoro barani Afrika, kukabiliana na changamoto za mabadiliko ya serikali yanayokiuka Katiba , ugaidi, na majanga ya asili yanayotokana na mabadiliko ya tabianchi, pamoja na changamoto za magonjwa na vitisho vya afya ya umma ambavyo vinatutaka tuwe na mshikamano ili kufanya juhudi zetu katika kutafuta mpango wa pamoja wa kuondoa matatizo," Lourenco amewaambia viongozi wa Afrika waliohudhuria mkutano huo wa AU.
Picha hii iliyopigwa Februari 14, 2025 ikimuonyesha Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa wa Djibouti Mahamoud Ali Youssouf (mbele) akiwa Addis Ababa, Ethiopia. (Xinhua/Liu Fangqiang)
Aidha mkutano huo umemchangua Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa wa Djibouti Mahamoud Ali Youssouf kuwa mwenyekiti mpya wa Kamati ya AU.
Youssouf, ambaye amechaguliwa mwenyekiti wa kamati hiyo ya awamu ya 2025-2028, badala ya Moussa Faki Mahamat, mwenyekiti anayemaliza muda wake na aliyekuwa waziri mkuu wa Chad, ambaye amemaliza muda wake wa awamu mbili za miaka minane akiongoza umoja huo wenye nchi wanachama 55.
Amewashinda Raila Odinga aliyekuwa Waziri Mkuu wa Kenya na Richard Randriamandrato aliyekuwa Waziri wa Mambo ya Nje wa Madagascar.
"Nafasi ya Afrika kwenye jukwaa la kimataifa itakuwa moja ya mambo yangu yatakayopewa vipaumbele. Afrika tunayoitaka ni Afrika yenye amani, ushirikiano na ustawi. Nikipewa nafasi ya kuwa mwenyekiti wa Kamati ya AU, nitajitahidi niwezavyo kuhakikisha bara letu linang'aa kwenye jukwaa la kimataifa," Youssouf alisema wakati akijinadi.
Mkutano huo wa siku mbili wa AU, uliofanyika kuanzia Jumamosi hadi Jumapili, umefanyika chini ya kaulimbiu ya AU ya mwaka 2025: "Haki kwa Waafrika na Watu Wenye Asili ya Kiafrika Kupitia Fidia."
people.cn © Tovuti ya Gazeti la Umma