

Lugha Nyingine
Waasi wa M23 wautwaa mji muhimu wa DRC huku mkutano wa AU ukionya hatari ya vita vya kikanda
Picha iliyopigwa Januari 30, 2025 ikionyesha mtaa wa Mji wa Goma, Jimbo la Kivu Kaskazini, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC). (Xinhua/Alain Uaykani)
KINSHASA – Kundi la M23 limetangaza Jumamosi kwamba wapiganaji wake wameingia Bukavu, mji mkuu wa Jimbo la Kivu Kusini, Mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) ambapo wakati mgogoro huo ukizidi kuongezeka, viongozi wa kikanda walikuwa wakikutana katika mkutano wa viongozi wakuu Umoja wa Afrika (AU) uliomalizika jana Jumapili, katika juhudi za kuzuia mgogoro huo usipanuke kuwa vita vikubwa zaidi vya kikanda.
Askari wakiwa katika ulinzi katika eneo la Lubero la jimbo la mashariki la Kivu Kaskazini, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC), Januari 14, 2025. (Picha na Zanem Nety Zaidi/Xinhua)
Uasi wa M23 waingia Bukavu
Kwenye taarifa iliyotolewa Jumamosi, Kundi la M23 limetoa wito kwa wakazi wa Bukavu kuunda "kamati za tahadhari ili kuhakikisha usalama na kuteua watu waadilifu na wenye kuwajibika kuwaongoza." Msemaji wa kundi hilo Laurence Kanyuka alithibitisha mapema siku hiyo kuwa M23 walikuwa wameingia mjini humo.
Siku ya Ijumaa, M23 ilitangaza kuwa imetwaa Uwanja wa Ndege wa Kavumba, kituo muhimu cha usambazaji wa misaada ya kibinadamu na kijeshi jimboni Kivu Kusini. Uwanja huo wa ndege unatumika kama safu kuu ya ulinzi ya Bukavu, mji ulio umbali wa kilomita 30.
Vyanzo vya habari nchini humo vimeliambia Shirika la Habari la China, Xinhua kuwa licha ya madai ya awali ya kundi hilo kwamba halikuwa na nia ya kuuteka mji huo, wapiganaji wake wameendelea kusonga mbele kuelekea Bukavu.
Wakati huo huo, baadhi ya wanajeshi wa DRC na washirika wao wameonekana wakirudi nyuma kuelekea Uvira, eneo la kimkakati la kibiashara na usafiri karibu na mpaka wa Burundi.
Mashambulizi hayo mpya ya M23 yamekuja wiki kadhaa baada ya kundi hilo kudai kuutwaa Goma, mji mkuu wa Jimbo la Kivu Kaskazini, Januari 26. Tangu mapema Februari, waasi hao wamekuwa wakitwaa miji kadhaa ya Kivu Kusini, ikizua hofu miongoni mwa wakazi wa Bukavu.
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres akizungumza kwenye ufunguzi wa Mkutano wa 38 wa Kawaida Baraza Kuu la Wakuu wa Nchi na Serikali wa Umoja wa Afrika (AU) mjini Addis Ababa, Ethiopia, Februari 15, 2025. (Xinhua/Han Xu)
Hatari ya mgogoro wa kikanda
Mapigano hayo ya Kivu Kusini, yakichochewa na kuendelea kwa mashambulizi ya M23, yanatishia kuipeleka kanda nzima ukingoni, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres ameonya siku ya Jumamosi kwenye mkutano wa AU mjini Addis Ababa, mji mkuu wa Ethiopia. Mgogoro huo unaozidi kuongezeka mashariki mwa DRC ulikuwa jambo kuu katika ajenda za mkutano huo.
Mapema mwezi Februari, Rais Evariste Ndayishimiye wa Burundi pia alionya kwamba mgogoro huo unaweza kuenea kuwa vita vya kikanda kama uhasama mashariki mwa DRC utaendelea. "Kama itaendelea namna hii, vita vina hatari ya kuenea katika kanda hiyo," alionya.
Watu waliolazimika kukimbia makazi yao wakiwasili kwa boti kwenye bandari ya Nzulo, karibu na Goma, Jimbo la Kivu Kaskazini, mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC), Januari 23, 2025. (Picha na Zanem Nety Zaidi/Xinhua)
Juhudi za upatishi wa kikanda zakwama
Siku ya Ijumaa, msemaji wa serikali ya DRC Tina Salama alithibitisha kuwa Rais Felix Tshisekedi hangeweza kuhudhuria mkutano huo wa kilele wa AU uliomalizika mwishoni mwa wiki, badala yake alimtuma Waziri Mkuu Judith Suminwa Tuluka kwenda mjini Addis Ababa.
Tshisekedi pia hakuwepo kwenye mikutano muhimu ya kikanda kuhusu mgogoro huo, ikiwa ni pamoja na mkutano wa viongozi wakuu ulioandaliwa wiki iliyopita na Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) na Jumuiya ya Maendeleo ya Kusini mwa Afrika (SADC) jijini Dar es Salaam, Tanzania.
Juhudi za kufikia makubaliano ya amani zimekuwa zikikwama mara kwa mara. Mwezi Desemba, mkutano wa kilele wa amani unaoongozwa na AU chini ya Mchakato wa Luanda, uliolenga kuwakutanisha pamoja Rais Tshisekedi na mwenzake wa Rwanda Paul Kagame kwenye meza ya mazungumzo, ulifutwa ghafla.
Rais Joao Lourenco wa Angola, mwezeshaji mteule wa Mchakato wa Luanda, ameshika wadhifa wa uenyekiti wa zamu AU kwa muhula wa mwaka mmoja siku ya Jumamosi. Akizungumza na waandishi wa habari, ameonyesha kufadhaika kutokana na kukwama kwa mazungumzo hayo lakini akasisitiza kuwa mazungumzo yanaendelea kuwa njia pekee mwafaka kuleta amani.
people.cn © Tovuti ya Gazeti la Umma