Jimbo la Gauteng la Afrika Kusini lasema liko tayari kuwa mwenyeji wa G20

(Tovuti ya Gazeti la Umma) Februari 19, 2025

JOHANNESBURG - Jimbo la Gauteng la Afrika Kusini liko tayari kuandaa Mkutano wa Kilele wa Viongozi Wakuu wa Kundi la 20 (G20) na kutumia fursa zinazoletwa na tukio hilo, amesema Vuyiswa Ramokgopa, ofisa wa Baraza Tendaji la Kilimo na Maendeleo Vijijini katika jimbo hilo la Gauteng.

Ramokgopa, ametoa kauli hiyo siku ya Jumanne kwenye uzinduzi wa G20 wa jimbo hilo akisema kuwa jimbo lake limeanza kuwa mwenyeji wa mikutano ya vikundi kazi vya G20 na liko tayari kuandaa Mkutano wa Kilele wa Viongozi Wakuu wa G20 mwezi Novemba 2025.

"G20 itakuwa chachu ya kutoa ajira endelevu na ukuaji wa uchumi katika jimbo, Afrika Kusini na Bara la Afrika. Tutatumia G20 kuonyesha utalii na ukarimu, utamaduni wa ujumuishaji, na Ubuntu (ubinadamu). Tutatumia G20 kumaliza njaa, ukosefu wa usawa na kuendesha ukuaji endelevu," amesema Ramokgopa.

Ameeleza kuwa wanaendelea kushirikisha mashirika ya kiraia, wafanyabiashara, vijana, na watu wenye ulemavu kuhusu G20 ili kusiwe na mtu anayeachwa nyuma, na wako tayari kukaribisha wageni.

"Waafrika Kusini wanajulikana sana kwa ukarimu wao katika kukaribisha wageni, na serikali inahimiza watu kufanya hivyo kama walivyofanya wakati wa Mkutano wa BRICS." amesema

Asharf Patel, mtafiti mwandamizi wa wanafikra bingwa wa Taasisi ya Mazungumzo ya Dunia, amebainisha kuwa G20 imezalisha ufuatiliaji na maslahi mengi kutoka kwa watu kutoka nyanja zote za maisha katika nchi za G20. Amesema Waafrika Kusini kuanzia wafanyabiashara, serikali na mashirika ya kiraia lazima wazungumze kwa sauti moja katika G20.

"Mihtasari zaidi ya 800 ya machapisho ya utafiti imepokelewa kutoka kwa watu kutoka nchi tofauti za G20, ambao ni sehemu ya T20 inayowakilisha wasomi na ni sehemu ya waandaaji."

Afrika Kusini imechukua urais wa zamu wa G20 na itakuwa mwenyeji wa Mkutano wa Kilele wa Viongozi Wakuu wa G20 mwezi Novemba. Jimbo hilo la Gauteng ni kitovu cha uchumi cha Afrika Kusini na ambalo lina watu zaidi ya milioni 15.

(Wahariri wa tovuti:Song Ge,Zhao Jian)

Picha