Uganda yawa na imani katika mapambano dhidi ya Ebola baada wagonjwa wote kuruhusiwa kutoka hospitalini

(Tovuti ya Gazeti la Umma) Februari 20, 2025

Wafanyakazi wa afya nchini Uganda wana imani kuwa nchi hiyo inaweza kuwa inaona mwisho wa mlipuko wa sasa wa Ebola baada ya kuruhusiwa kutoka hospitalini kwa wagonjwa wote waliokuwa wameambukizwa ugonjwa huo.

Jane Ruth Aceng, waziri wa afya wa Uganda, na Kasonde Mwinga, mwakilishi wa Shirika la Afya Duniani (WHO) nchini Uganda, waliongoza hafla ya kuruhusiwa kutoka hospitalini kwa wagonjwa hao Jumanne mjini Kampala.

Aceng amesema wagonjwa wanane, saba mjini Kampala na mmoja katika wilaya ya mashariki ya Mbale, wameruhusiwa kutoka hospitalini, baada ya kupitia siku 21 za matibabu.

Watu tisa walithibitishwa kuambukizwa ugonjwa huo nchini Uganda, ikiwa ni pamoja na kifo kimoja, tangu mlipuko huo wa hivi karibuni ulipotangazwa mnamo Januari 30.

Shirika la Afya Duniani (WHO) limeelezea kuruhusiwa huko kwa wagonjwa kutoka hospitalini kama hatua muhimu katika juhudi za pamoja za kuzuia kuenea kwa ugonjwa huo na kumaliza mlipuko huo.

“Lazima tuendelee kufanya kazi na idara husika za kitaifa ili kuhakikisha kuwa mwitikio wetu unaendelea kuwa juu. Siku 42 zijazo ni muhimu katika kuhakikisha hakuna kisa kipya kinachotokea," amesema Mwinga, mwakilishi wa Shirika la Afya Duniani. "Kama hakuna maambukizi mapya yatakayotokea katika kipindi hiki, mlipuko huu utatangazwa kuwa umeisha."

Shirika la Afya Duniani limehimiza umma dhidi ya kunyanyapaa watu walioambukizwa na kupona Ebola, likisisitiza kuwa wako "salama, hawawezi tena kuambukiza na hawana hatari kwa afya kwa wengine."

(Wahariri wa tovuti:Zhou Linjia,Zhao Jian)

Picha