

Lugha Nyingine
Baraza la Mawaziri la Afrika Kusini lasema amri tendaji ya Marekani "imejawa habari potofu"
Watu wakionekana kwenye mtaa wa kibiashara mjini Cape Town, Afrika Kusini, Novemba 28, 2021. (Xinhua/Lyu Tianran)
JOHANNESBURG - Serikali ya Afrika Kusini kupitia taarifa iliyotolewa na Baraza lake la Mawaziri imekataa madai yaliyotolewa katika amri tendaji iliyotiwa saini na Rais wa Marekani Donald Trump hivi karibuni kuhusu 'kuwatendea vibaya na kutwaa ardhi' watu wa jamii ya wazungu Waafrikana, ikiyaelezea kuwa "yamejaa habari potofu."
Taarifa hiyo ya Baraza la Mawaziri la nchi hiyo, iliyotolewa Alhamisi, imekuja baada ya Trump kutia saini amri tendaji mapema mwezi huu ya kukata msaada wa kifedha kwa Afrika Kusini, akirejelea kutokubaliana na sera yake ya ardhi na kuishutumu nchi hiyo "kutwaa mali ya kilimo ya jamii ya Waafrikana walio wachache."
"Amri hiyo tendaji inakosa ukweli wa mambo na inatokana na habari potofu na uongo unaolenga kutoeleza madhumuni halisi ya sheria na kusababisha mgawanyiko wa matabaka ya rangi katika taifa letu." imesema taarifa hiyo.
Imetoa wito kwa raia kuiunga mkono nchi hiyo dhidi ya kile ilichokieleza kuwa habari potofu kuhusu Afrika Kusini.
Picha ikionyesha mtaa usio na watu mjini Johannesburg, Afrika Kusini, Aprili 17, 2020. (Picha na Zodidi Mhlana/Xinhua)
“Kwa kuzingatia hali yetu ya zamani, hatuwezi kufumbia macho ukiukwaji wa haki za binadamu unaofanywa kote duniani, wala hatuwezi kuwapuuza watu walio katika hali mbaya wanaohitaji sauti yetu kuwapunguzia mateso,” imesema taarifa hiyo.
Pia imezungumzia Muswada wa Sheria ya Kutwaa Ardhi kwa Matumizi ya Umma, ambao hivi majuzi ulitiwa saini kuwa sheria na ulionekana kutoleta utulivu kwa serikali ya Marekani kwa vile unaruhusu taasisi za umma kuchukua ardhi kwa maslahi ya umma.
"Baraza la Mawaziri limekataa madai kwamba serikali ya Afrika Kusini inatwaa ardhi na 'kuwatendea watu wa tabaka fulani vibaya sana.' Afrika Kusini ni demokrasia ya kikatiba ambayo ina dhamira thabiti katika kulinda haki za watu wote wanaoishi nchini kwa mujibu wa Kifungu cha Haki na Katiba," imesema taarifa hiyo.
Kuhusu kujiondoa kwa Marekani kwenye Mpango wa Dharura wa Kukabiliana na Ukimwi (PEPFAR), Baraza hilo la Mawaziri limesema Afrika Kusini ilikuwa ikitumia randi bilioni 46.8 (dola za Kimarekani karibia bilioni 2.56) katika mwaka wa fedha wa 2024/2025 kwa matibabu ya antiretroviral, huku asilimia 17 tu ya fedha hizo zikitoka Marekani.
“Fedha za PEPFAR hutumika tu kwa mishahara na gharama za uendeshaji kwa watu waliowateua moja kwa moja katika wilaya 27,” imesema taarifa hiyo.
people.cn © Tovuti ya Gazeti la Umma