

Lugha Nyingine
Kampuni binafsi za China zapiga hatua katika biashara ya nje mwaka 2024
Picha ikionyesha magari ya abiria yanayosubiria kusafirishwa katika bandari mjini Lianyungang, Mkoani Jiangsu, Mashariki mwa China, Februari 21, 2025. (Picha na Wang Chun/Xinhua)
BEIJING – Kampuni binafsi za China zimeendelea kuwa kundi linaloongoza la uendeshaji biashara ya nje nchini humo kwa miaka sita mfululizo, zikipata mafanikio makubwa kwenye biashara ya nje katika kipindi cha mwaka 2024, takwimu za Mamlaka Kuu ya Forodha ya China zimeonyesha.
Taarifa ya mamlaka hiyo inaonesha kuwa, mafanikio hayo yanajumuisha idadi ya kampuni binafsi zinazofanya shughuli za kuagiza na kuuza bidhaa nje kupita jumla ya 600,000 kwa mara ya kwanza katika mwaka 2024, ikifikia 609,000 mwaka jana.
Inaeleza kuwa, kampuni hizo binafsi za China pia ziliibuka kuwa wafanyabiashara wakubwa zaidi wa bidhaa za teknolojia ya hali ya juu nchini humo, huku sehemu yao ikipanda kwa asilimia 3 hadi asilimia 48.5 ya jumla ya biashara ya teknolojia ya hali ya juu ya China mwaka 2024.
Aidha, mamlaka hiyo ya forodha imeeleza kuwa, kampuni hizo binafsi kwa mara ya kwanza zilichukua zaidi ya nusu ya uagizaji nje wa bidhaa za wanunuzi nchini China, huku sehemu yao ikipanda kwa asilimia 2.8 hadi asilimia 51.3 -- hasa ikizidi asilimia 60 katika kategoria kama vile vipodozi na matunda.
Mamlaka hiyo pia imeeleza kuwa, kampuni binafsi za China ziliendelea kuongoza biashara ya nje ya nchi hiyo kwa miamala ya jumla yenye thamani ya yuan trilioni 24.33 (dola za Kimarekani karibu trilioni 3.4) mwaka jana, zikirekodi ongezeko la asilimia 8.8 kuliko mwaka jana na kuchukua asilimia 55.5 ya jumla ya thamani ya biashara ya nje ya nchi hiyo.
Wakati huo huo, mamlaka hiyo ya forodha ya China imesema, kampuni zilizowekezwa kwa mtaji wa kigeni zilirekodi biashara ya yuan trilioni 12.8 mwaka jana, ongezeko la asilimia 1.5, huku kasi ya biashara yao ikiongezeka katika nusu ya pili ya mwaka 2024.
“Kampuni zinazomilikiwa na serikali ya China zilichangia yuan trilioni 6.61 katika biashara ya nje, zikitoa mchango muhimu katika kuagiza kutoka nje bidhaa za kimkakati, zikiwemo nafaka na rasilimali za nishati” mamlaka hiyo imeeleza.
Imeeleza kuwa, jumla ya idadi ya kampuni zilizo na shughuli za kuagiza na kuuza nje bidhaa katika sekta binafsi, zinazowekezwa na mtaji wa kigeni na zile zinazomilikiwa na serikali ilifikia rekodi ya juu ya karibu kampuni 700,000 katika mwaka 2024.
people.cn © Tovuti ya Gazeti la Umma