Ethiopia na Somalia kuimarisha ushirikiano wa kijeshi katika mapambano dhidi ya ugaidi

(CRI Online) Februari 25, 2025

Kwa mujibu wa taarifa ya pamoja iliyotolewa Jumamosi mwishoni mwa wiki iliyopita, Ethiopia na Somalia zinapanga kuanzisha “Hadhi ya Makubaliano ya Kikosi cha Kijeshi” kwa vikosi vyao vya pande kitakachokuwa na makao yake makuu nchini Somalia.

Makubaliano hayo yanakuja kufuatia mazungumzo kati ya Waziri Mkuu wa Ethiopia, Abiy Ahmed na Rais wa Somalia Hassan Sheikh Mohamud yaliyofanyika Addis Ababa Februari 14-16, na majadiliano yaliyofuata kati wakuu wa majeshi ya nchi hizo mbili yaliyofanyika siku hiyo ya Jumamosi.

Ujumbe ulioongozwa na mkuu wa majeshi ya Jeshi la Ulinzi la Taifa la Ethiopia Birhanu Jula ulifanya ziara ya kikazi nchini Somalia Jumamosi mwishoni mwa wiki iliyopita ukifanya mazungumzo na maofisa wa Somalia akiwemo mkuu wa Jeshi la Ulinzi la Somalia Odowaa Yusuf Rageh juu ya njia za kuimarisha ushirikiano wa pande mbili katika mapambano dhidi ya kundi la Al-Shabaab, na kudumisha amani, usalama na utulivu katika Pembe ya Afrika.

Taarifa hiyo ya pamoja pia imeeleza kuwa wakuu hao wa majeshi ya nchi hizo mbili wamepongeza ujumbe wa Umoja wa Afrika wa Uungaji Mkono na Kuleta Utulivu Somalia (AUSSOM) kwa kuanza kazi yake nchini humo na kusisitiza umuhimu wa kuendeleza mafanikio yaliyofikiwa na mtangulizi wake Ujumbe wa Mpito wa Umoja wa Afrika nchini Somalia (ATMIS).

(Wahariri wa tovuti:Song Ge,Zhao Jian)

Picha